DC ataka hatua upatikanaji maji Saranga, Kinyerezi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:47 PM Feb 10 2025
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Lazaro Twange
Picha: Mtandao
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Lazaro Twange

MKUU wa Wilaya ya Ubungo, Lazaro Twange, amewataka watendaji wa DAWASA Kinyerezi kuhakikisha wanawapatia huduma ya maji wakazi wa Saranga Mpakani, waliosota kwa muda wa takriban miaka miwili, bila maji kutoka kwenye mabomba

Amesema atarudi Saranga Mpakani wiki ya kwanza ya Machi 2025, kama walivyoahidi watendaji hao kwamba tatizo la Saranga litamalizwa mradi wa Bangulo utakapokamilika.

Twange alitoa kauli hiyo juzi, wakati akihitimisha mazungumzo yake na wananchi wa Saranga Mpakani, alipokwenda kusikiliza kilio cha wananchi hao ambao wana ukosefu wa huduma ya maji ya bomba kwa kipindi kirefu sasa.

Baada ya kuwasikiliza wananchi wa Mtaa wa Saranga Mpakani, DC Twange alimtaka Meneja wa DAWASA Kinyerezi kwa upande wake kama yaliyoelezwa na wananchi anayafahamu na kwa kiasi gani wameyatafutia ufumbuzi.

Meneja wa DAWASA Kinyerezi, Cosman Makero, alisema ni kweli kero za ukosefu wa huduma ya maji kwa wananchi hao anazifahamu na kuwaomba wawe wavumilivu kwani mwanzoni mwa Machi, mwaka huu, wataanza kupata maji ya uhakika.

Alisema Kata ya Saranga, kwa ujumla ina changamoto ya ukosefu wa maji kwa muda mrefu na kwamba hali hiyo inachangiwa na mahitaji ya maji kuwa kubwa kutokana na wingi wa watu.

Aidha, alisema baada ya kuona tatizo hilo na kwamba DAWASA inajenga tangi kubwa la maji eneo la Bangulo, Hali ya Hewa Wilaya ya Ilala na kwamba tayari ujenzi wake umekamilika.

Meneja huyo alisema ujenzi wa tangi hilo, umekamilika wanachoendelea nacho kwa sasa ni kulaza mabomba kwenda eneo la Saranga Mpakani na kwamba wameshalaza mabomba kilometa tatu, bado tatu kukamilisha ulazaji huo.

"Mwinzoni mwa mwezi ujao (Machi), tutakuwa tumekamilisha. Hata hivyo, kwa kuwa wananchi hawana maji tumeona tulete tangi, ili wakazi wa eneo hili wawe wanakuja kuchota kwa ndoo hapa ofisi za serikali ya mtaa," alisema Makero.

Awali, mkazi wa Saranga Mpakani, Emmanuel Shio, alieleza tatizo la maji lilianza miaka miwili iliyopita, baada ya kuhamishwa kutoka kuhudumiwa na DAWASA Kimara Wilaya ya Ubungo na kuanza kuhudumiwa na DAWASA Kinyerezi iliyopo Wilaya ya Ilala.

"Tunalazimika kununua kwenye maboza ambao nao ukiagiza wanataka lazima ununue kuanzia lita shilingi 3,000 ambazo wanauza kwa jumla ya shilingi 45,000 kinyume na hapo hawakuletei.

"Kwa hali iliyopo na usanii wa maofisa wa DAWASA Kinyerezi, tunaomba turudishwe kuhudumiwa na DAWASA Kimara. Hili tangi waliloleta hawa watu wa DAWASA hapa serikali ya mtaa ni kutaka kuvuruga ndoa za watu na watoto wa kike kubakwa. 

"Hapa kina mama waamka usiku kuja kupanga foleni ya kuchota maji. Kuna watu wamekuja alfajiri hapa, lakini sasa hivi ni saa sita kasoro mchana, hawajapata maji hata ndoo moja. 

“Kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kumtua mama ndoo kichwani. Hawa DAWASA Kinyerezi wanakuja na hili tangi ili kumtwisha Mama ndoo kichwani. Tunaomba hili tangi hata kama litakuwepo lakini hitaji ni mabomba yatoe maji," alisisitiza.

Pamoja na hayo, Shio pia alimwomba Mkuu wa Wilaya ambaye alikuwa ameambatana na ofisa kutoka TARURA Ubungo, kupitisha greda katika barabara ya kutoka kwa Hunju mpaka kwa Mbunguli, ili ionekane ni barabara tofauti na ilivyo sasa.

Mkazi mwingine wa Saranga Mpakani, Hafsa Hussein, alisisitiza kuwa wanataka maji yatoke kwenye mabomba yao nyumbani na si kuwekewa tangi.

"Kuna siku tuliandamana kwenda DAWASA Kinyerezi maji yakatoka, sasa hayo yaliyotoka yalitoka wapi? Huko kwenye mabonde tukiwatuma watoto wanabakwa tumechoka na hii hujuma tunayofanyiwa," alisema.

Baada ya maelezo hayo Mkuu wa Wilaya aliwapa pole wananchi kutokana na kadhia hiyo na kueleza kuwa meneja wa DAWASA Kinyerezi ameeleza mengi, lakini kubwa ni kwamba wapo mbioni kukamilisha mradi wa Bangulo na ndipo maji yatafika huku kwa wingi.

"Kwa muda wangu nitakwenda kujionea walipofikia nanyi niwaombe mjitokeze watu wawili au watatu mkaangalie hiki kinachoelezwa hapa. Hili la barabara naomba meneja wa TARURA, lishughulikie kwa kuwapatia greda lije lichonge hii barabara si lipo ndani ya uwezo wako kama huna uwezo nalo niambie nikatafute kwingine," alisema Lwanga.

DC Twange amehamishiwa Wilaya ya Ubungo, mwishoni mwa Januari, akitokea Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, ambako alikuwa akihudumu kwa nafasi hiyo ya mkuu wa wilaya.