Imebainika kuwa barabara inayoelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga haikuwahi kuingizwa kwenye mpango wa bajeti ya Serikali, hali inayosababisha madhara kwa wagonjwa na watumiaji wengine wa barabara hiyo kutokana na ubovu wake.
Barabara hiyo imekuwa chanzo cha ajali mbaya, ikiwemo ile ya Mei 9 mwaka jana, ambapo mapacha wawili, Dotto Mahenga na Kulwa Mahenga kutoka Kijiji cha Lyandu, Manispaa ya Shinyanga, walifariki dunia baada ya kugongwa na gari lililokuwa likikwepa mashimo wakiwa kwenye pikipiki.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Annamringi Macha, amesema ucheleweshaji wa ujenzi wa barabara hiyo unatokana na kutokuwekwa kwenye bajeti ya Serikali. Hata hivyo, viongozi wa mkoa wamekuwa wakitoa maagizo kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kufanya ukarabati wa muda kwa kuziba mashimo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya.
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, amesema kuwa barabara hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto za kibajeti, huku ikiingiliwa na ahadi za viongozi mbalimbali.
“Kero kubwa iliyosalia ni ujenzi wa barabara hii ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Endapo fedha kutoka Benki ya Dunia zitachelewa kuingia, italazimu kuiingiza kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026,” alisema Katambi.
Kupitia Tovuti ya Bunge, Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mnzava, aliuliza swali bungeni Novemba mwaka jana kuhusu lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Zainab Katimba, alisema kuwa barabara hiyo ipo kwenye mpango wa Serikali na itajengwa kwa kiwango cha lami mara fedha zitakapopatikana.
“Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa barabara hii ipo kwenye mpango wa Serikali, na dhamira yetu ni kuhakikisha inajengwa kwa kiwango cha lami ili iweze kuwanufaisha wananchi,” alisema Katimba.
Katika bajeti ya TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kiasi cha Shilingi bilioni 841.19 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi, matengenezo, na ukarabati wa barabara. Hata hivyo, barabara ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga haijajumuishwa kwenye bajeti hiyo.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Shinyanga, Mhandisi Samson Pamphil, amesema barabara hiyo haikuwa kipaumbele cha Serikali kutokana na ufinyu wa bajeti. Hata hivyo, baada ya kupatikana kwa Shilingi bilioni 9 kutoka Benki ya Dunia, ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami unatarajiwa kuanza mwezi Machi mwaka huu.
Sera ya Afya ya mwaka 1990, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2007, inasisitiza upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wote kwa urahisi.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Luzila John, amesema kuwa hali ya barabara hiyo ni hatari kwa wagonjwa, hususan wale waliopitia upasuaji wa mifupa na wajawazito.
“Mjamzito au mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa mifupa anapaswa kuwa na uangalizi wa hali ya juu. Kupita kwenye barabara yenye mitikisiko ni hatari kwa afya yake na inaweza kusababisha mimba kuharibika au kujifungua njiani,” alisema Dk. Luzila.
John Maige, mkazi wa Mwawaza, alieleza kusikitishwa kwake na hali ya barabara hiyo:
“Naishangaa sana Serikali, barabara ya hospitali ambayo ni muhimu kwa wananchi haipewi kipaumbele, lakini barabara zisizo za muhimu zinajengewa lami upya,” alisema Maige.
Mgonjwa Stella Paulo alisimulia jinsi alivyosumbuka alipokuwa akienda hospitalini kwa usafiri wa bodaboda:
“Barabara hii ni mbovu sana, lakini sisi wanyonge hatuna namna, lazima tuje hapa kupata matibabu. Lakini kungekuwa na hospitali kubwa hata ya binafsi hapa Shinyanga, nisingekuja huku – ni mateso juu ya mateso,” alisema Stella.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amesema kuwa kutokana na umuhimu wa barabara hiyo, wamekuwa wakitoa maelekezo kwa TARURA kufanya ukarabati wa muda kwa kuziba mashimo wakati wakisubiri fedha kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa lami.
“Barabara hii ni ya muhimu kwa sababu inahusiana moja kwa moja na maisha ya wananchi. Tumekuwa tukifukia mashimo ili kupunguza madhara kwa wagonjwa wakati tukisubiri utekelezaji wa ujenzi kwa kiwango cha lami,” alisema Mtatiro.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED