Fursa tele zaanikwa Bwawa la Kidunda

By Ida Mushi ,, Frank Monyo , Nipashe
Published at 09:49 AM Feb 10 2025
Ujenzi Bwawa la Kidunda.

UJENZI wa Bwawa la Kidunda lenye uwezo wa kutunza lita za maji bilioni 190, pindi utakapokamilika Juni mwakani, utasaidia kipindi cha kiangazi kuwa na uhakika wa upatikanaji maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani.

Bwawa hilo mbali na kuhifadhi maji, litakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa maji MW 20 kwa ajili ya kuingizwa katika Gridi ya Taifa na matumizi ya maeneo ya karibu na mradi pamoja na kusaidia umwagiliaji, ukiwamo uzalishaji miwa katika kiwanda cha sukari Mkulazi Na. 1.

Hayo yalielezwa na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mkama Bwire mwishoni mwa wiki wakati wahariri na waandishi waandamizi kutoka vyombo mbalimbali vya habari walipotembelea wilayani Morogoro kuona maendeleo ya ujenzi huo utakaogharimu Sh. bilioni 336.

Bwire alisema kuwapo mradi huo kumewezesha utekelezaji mradi wa barabara zaidi ya kilomita 75 kwa kiwango cha changarawe kutoka Ngerengere hadi Kidunda.

"Ujenzi wa barabara hii nao unasaidia kuinua hali ya uchumi ya watu ambao wapo kando ya barabara, kama mnavyoona huku vijijini shughuli za kilimo zinaendelea, hivyo watu wataweza kuzalisha mazao yao na kuweza kuyafikisha kwenye masoko," alisema. 

Bwire aliongeza kuwa kuwapo bwawa hilo kutasaidia jamii ambayo ipo kwenye maeneo hayo, kufanya shughuli za uvuvi kulingana na taratibu zitakazowekwa na Wizara ya Uvuvi. Pia kutakuwa na shughuli za kitalii.

"Kwa hiyo hayo ni baadhi tu ya manufaa tunayoyaona ya moja kwa moja ukiachana na faida zingine za watu watakaohusika katika shughuli za ujenzi na ajira," alisema.

Kaimu Mtendaji huyo wa DAWASA alikiri kuwa kwa siku za karibuni, Jiji la Dar es Salaam limekumbana na changamoto katika upatikanaji maji ya uhakika, hususani kipindi cha kiangazi, hivyo kukamilika kwa ujenzi wa bwawa hilo kutawezesha uboreshaji huduma ya majisafi na salama na hatimaye kuwa na uhakika wa maji.

Alisema tangu Uhuru wa nchi mwaka 1961, mipango ya ujenzi wa bwawa hilo ilikuwa kwenye karatasi, lakini serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetekeleza kwa vitendo na kwa sasa ujenzi wake umefikia zaidi asilimia 27.

"Bwawa la Kidunda liko katika mkondo wa Mto Ruvu na ndio chanzo kikubwa cha maji katika maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ambapo zaidi ya asilimia 87 ya maji yote yanayozalishwa katika eneo la Ruvu yanategemea na mto huo na bwawa hili litasaidia sana kuhifadhi maji wakati wa mvua na kutumika kipindi cha kiangazi," alisema Bwire.

Aliongeza kuwa kutokana na changamoto ambayo imekuwa inajitokeza mara kwa mara katika miaka ya nyuma ya kupungua kwa kina cha Mto Ruvu kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, kumekuwa kunatokea madhara makubwa kwenye uzalishaji maji na kuathiri upatikanaji wa huduma ya maji kwa matumizi ya binadamu na kiuchumi kwa wanaotegemea chanzo hicho cha maji.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, Janeth Kisoma ambaye pia ni Meneja Sehemu ya Mazingira na Uratibu wa Jumuiya za Watumia Maji kutoka bonde hilo, alisema bwawa hilo ni miongoni mwa vyanzo vya maji vinavyosimamiwa bonde hilo na mipango iliyopo ya kulilinda ni kulitangaza kuwa eneo tengefu la hifadhi kwenye Gazeti la Serikali.

"Bodi imekuwa inashirikiana na wadau mbalimbali katika kuhifadhi mazingira na mpaka sasa tumejenga zaidi ya mabirika 29 ya kunyweshea mifugo kwenye vijiji vinavyozunguka Mto Ruvu ili mifugo isiingie mtoni na kuharibu chanzo hicho cha maji," alisema.

Aliongeza kuwa jukumu lililopo sasa ni kulinda, kutunza na kuhifadhi  vyanzo vya maji chini ya usimamizi wa Sheria ya Rasilimali za Maji Na. 11 ya Mwaka 2009 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022 na kwamba bodi hiyo inasimamia vyanzo vya maji 283, yakiwamo mbwawa, visima, mito, chemichem na maeneo mengine.

Alisema watumiaji wa vyanzo vya maji ni wengi hivyo ni lazima  wasimamie na kuweka taratibu ili wanaotaka kupata huduma za maji zikiwamo shughuli za kilimo, umeme na matumizi majumbani, Ni lazima waombe vibali ili kila mtumiaji apate kiasi cha maji mengine yabaki katika mito kwa matumizi mengine.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alisema kuwa kwa muda mrefu vyombo vya habari vimekuwa vinaandika juu ya ukame, upungufu wa maji, mgawo wa maji katika Jiji la Dar es Salaam lakini mara kwa mara vimekuwa vinarejea suluhisho la tatizo hilo ni ujenzi wa Bwawa la Kidunda.

Alisema baada ya vyombo vya habari kuandika kwa mfululizo habari za malalamiko kuhusu kero ya maji, serikali chini ya Rais Samia ilisikia  kilio hicho na kuanza ujenzi wa mradi huo mkubwa ambao unatarajiwa kuwa mkombozi wa muda mrefu wa maji hasa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Balile alisema wanaamini serikali itaendelea kujenga miradi mikubwa kama wa Kidunda inayohitaji fedha na utaalamu katika maeneo mbalimbali nchini ili kutatua kero za wananchi na kutimiza vyema wajibu wake wa kuwahudumia wananchi kwa kuhakikisha wanapata huduma za kijamii.