WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema serikali imelipa takribani Sh. bilioni 254 ndani ya miezi miwili kwa wakandarasi mbalimbali wanaotekeleza miradi ya barabara na madaraja nchini baada ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Ulega ameyasema hayo leo jijini Dodoma baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Ntyuka hadi Kikombo yenye urefu wa kilomita 76 inayojengwa kwa awamu mbili na wakandarasi wawili ambao ni CHICO na China First.
Waziri huyo amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo ya kulipwa kwa wakandarasi hao, ili kuwajengea uwezo wa kukamilisha miradi yote ya sekta ya ujenzi kutekelezwa kama ilivyopangwa.
“Mmeona katika muda wa hii miezi mwili Rais Samia tayari amelipa malipo ya wakandarasi ya takribani Sh. bilioni 254, matumaini yetu tunataka kuona kazi zikiendelea,” amesema Ulega.
Ameongeza kuwa mwishoni mwa Februari mwaka huu, serikali inatarajia kutoa fedha nyingine za kutekeleza miradi ya miundombinu katika sekta ya ujenzi, huku akiiagiza Waka wa Barabara Tanzania (TANROADs) kuipa kipaumbele barabara hiyo ili ianze kujengwa haraka.
Naye, Waziri wa Madini ambaye ni Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde, amesema kutokana na umuhimu wa barabara ya Ntyuka Kikombo ni muhimu kuikamilisha kwa kiwango cha lami kwakuwa ni mkombozi kutokana na uwepo wa hospitali kubwa ya macho ya Mvumi inayotoa huduma nchi nzima na pia kuunganisha maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Mtendaji Mkuu wa (TANROADS) Mhandisi Mohammed Besta, amesema ujenzi wa barabara hiyo unatekelezwa kwa sehemu mbili ambako ya kwanza ni kutoka Ntyuka, Mvumi hadi Makulu, na nyingine inaanzia Kikombo inapita Chololo hadi Mapinduzi ikiwa na urefu wa kilomita 25.
“Mradi wa ujenzi wa barabara hizo unatekelezwa na Mkandarasi CHICO kwa gharama ya Sh. Bilioni 38.1 na sehemu ya pili ya Ntyuka hadi Kikombo inatekelezwa na China First kwa gharama ya Sh. Bilioni 98.4,” amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED