Samia Legal Aid yapata matokeo chanya K’njaro

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 01:37 PM Feb 10 2025
Mratibu wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Murumbe Daudi.
Picha: Mtandao
Mratibu wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Murumbe Daudi.

KAMPENI ya Msaada wa Kisheria ya Samia Legal Aid, imepata matokeo chanya katika Mkoa wa Kilimanjaro, baada ya kuwafikia wananchi wasio na uwezo 121,000 waliowasilisha migogoro 740, huku ikifanikiwa kutatua migogoro 94.

Migogoro 646 iliyosalia, inaendelea kufanyiwa kazi na jopo la mawakili linalofanya kazi na kampeni hiyo inayoendeshwa na Wizara ya Katiba na Sheria, kuhudumia wananchi katika ngazi mbalimbali.

Akizungumza jana katika Mji wa Moshi, wakati wa makabidhiano ya ripoti ya utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa Mkoa wa Kilimanjaro, Mratibu wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Murumbe Daudi, amesema malalamiko makubwa waliyoyapokea ni ya ardhi.

“Tulianza kampeni hii ya Huduma za Msaada wa Kisheria Mkoa wa Kilimanjaro, Januari 29 na Februari 7 mwaka huu, tumehitimisha huduma hii ya kutoa huduma kwa wananchi tulioweza kuwafikia ni 121,000.

“Migogoro 740 tumeipokea, tumetatua migogoro 94 wa ndani pamoja na wenzetu waliokuwa maeneo hayo na imeonyesha ni mafanikio lakini pia ile ambayo imesalia migogoro 600 na kitu inaendelea kufanyiwa kazi pamoja na wale mawakili wetu wanaoendelea kuhudumia wananchi katika ngazi mbalimbali.

…Lakini pamoja na hayo, wale wananchi waliotufikia wameisifia huduma hii, wameipongeza na tunaendelea kuwasiliana nao wale ambao wanaendelea kutatuliwa changamoto zao.”

Kwa mujibu wa Murumbe, chanzo cha migogoro hiyo Kilimanjaro, jopo la mawakili limebaini inatokana na uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya ardhi.

“Bado uelewa wa wananchi wetu ni mdogo kuhusu masuala ya ardhi. Ni namna gani mtu atwae ardhi, namna gani inaweza kuhamishwa ardhi kwenda kwa mtu mwingine. Mingine inasababishwa na vurugu tu, kati ya familia na familia. Kuna migongano ya familia na mingine ni mambo ya mirathi,”amesema Mratibu huyo.

Januari 29 mwaka huu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, alieleza kuwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, lengo lake kuu ni kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati, hasa kwa wananchi wanyonge.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, alitangaza kuchukuliwa hatua kali kwa watu wote wanaokiuka sheria, haki za binadamu, wanaonyang'anya watu haki za mirathi, wanaosababisha migogoro ya ardhi pamoja na wanaoendeleza ukatili wa kijinsia.