THRDC yabainisha athari tisa USAID kusitisha msaada

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:02 PM Feb 10 2025
Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa
Picha: Mtandao
Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRC), umetaja athari tisa zilizosababishwa na uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump kulifuta Shirika la Misaada la Marekani (USAID), ambazo zinatakiwa kuwekewa mkakati wa kuzikabili kupunguza madhara kwa Watanzania.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa kurasa saba, uliofanywa na Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, utafiti unaonesha kuwa kusitishwa ghafla kwa ufadhili wa Marekani, tayari kumesababisha madhara makubwa kwa mashirika yaliyopewa taarifa rasmi za kusimamia miradi yote inayotegemea fedha za Marekani.

Amezitaja athari hizo ni kuachishwa kazi kwa wafanyakazi mashirika mengi, hasa yale yaliyotegemea kwa asilimia 100 ufadhili wa serikali ya Marekani, ambayo yamelazimika kupunguza wafanyakazi wake.

Pia zingine ni kusitishwa kwa miradi mingi inayoendelea, kukatishwa ghafla kabla ya kukamilika ambako kuna athari kwa wanufaika.

Zingine anasema ni madhara kwa wanufaika wa miradi makundi yaliyo hatarini yameathirika kwa kiasi kikubwa, kama vile watoto waliokuwa wakisaidiwa kielimu, vituo vya hifadhi salama kwa watoto, wanawake, wazee, watu wenye ulemavu, watu wanaoishi na VVU/UKIMWI na wanafunzi waliopata ufadhili wa masomo.

Pia kupotea kwa ajira kwa maelfu ya Watanzania, wafanyakazi wa mashirika yaliyoathirika wanakabiliwa na hatari ya kukosa ajira, migogoro ya kimkataba mashirika huenda yakakumbwa na migogoro na washauri wa miradi na watoa huduma waliokuwa wameingia mikataba kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Pia, kupungua kwa mapato ya serikali kupitia kodi serikali itakosa mapato yaliyotokana na kodi ya ajira na mzunguko wa fedha katika uchumi, mtikisiko wa kiuchumi kwa wafanyakazi waliopoteza kazi na ajira au walioko katika hali ya hatari wanakumbwa na changamoto za kifedha kutokana na kusitishwa ghafla kwa ufadhili, jambo ambalo halikuzingatia taratibu za kawaida za kusitisha mikataba ya ajira.

Aidha, kupungua kwa mchango wa asasi za kiraia katika uchumi wa taifa, akisema utoaji wa fedha za misaada kutoka Marekani ulikuwa na mchango mkubwa katika sekta ya ajira, maendeleo na fedha za kigeni, hivyo kupunguzwa kwake kutasababisha mdororo mkubwa wa sekta hiyo.

Kadhalika alitaja zingine ni upotevu wa takribani dola bilioni tatu, ambazo Tanzania imenufaika nazo kila mwaka kutoka misaada ya Marekani, ikijumuisha fedha zilizotengwa kwa mashirika ya kiraia, idara za serikali na makampuni binafsi yanayofanya kazi nchini Tanzania.

“Kupungua kwa mzunguko wa dola za Marekani nchini kwa kuwa kusitishwa kwa ufadhili huu kutaathiri upatikanaji wa fedha za kigeni ndani ya nchi, kusitishwa kwa fedha za miradi ya 2024 ambayo ni takribani dola milioni 500 zilizokuwa zimetengwa kwa miradi ya mashirika ya kiraia, makampuni, na miradi mingine ya maendeleo mwaka 2024 zitabaki zimeganda hadi kutakapopatikana maelekezo mapya kutoka kwa serikali ya Trump.

“Kwa mwaka 2023 Tanzania ilipokea Dola milioni 630 (sawa na Sh. Trilioni 1.61) na kuifanya kuwa miongoni mwa nchi 20 zilizoongoza kwa kupokea misaada kutoka USAID huku ikishika nafasi ya 10 duniani na ya 10 barani Afrika,” amebainisha.