WAKATI kikosi cha Yanga kinatarajia kuondoka nchini leo kuelekea Mauritania kuifuata Al Hilal kwa ajili ya mechi ya raundi ya tano ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kiungo nyota, Maxi Nzengeli, hatakuwa sehemu ya mchezo huo.
Mbali na Nzengeli, Yaou Kouassi na Aziz Andambwile, pia wanabakia nchini kutokana na kutokuwa fiti kuwakabili vinara hao wa Kundi A.
Al Hilal itaikaribisha Yanga katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Jumapili kuanzia saa 4:00 usiku kwa saa za Tanzania.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Novemba 26, mwaka jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga walikubali kipigo cha mabao 2-0.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, alisema mchezo huo ni muhimu zaidi kwao katika mbio zao za kusaka tiketi ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Ramovic alisema wanakwenda Mauritania wakitambua wanatakiwa kupata ushindi kwa sababu wanafahamu wakipoteza mchezo huo watakuwa wamejiweka katika hali ngumu kwenye mbio za kusonga mbele katika michuano hiyo.
"Ni mchezo tunaohitaji zaidi ushindi, hautakuwa mchezo mwepesi lakini tumejiandaa vizuri, kikubwa kila mchezaji anafahamu sehemu tulipo na nini tunatakiwa kufanya, tupo tayari kupambania nafasi yetu ya kucheza robo fainali," alisema Ramovic.
Aliongeza wachezaji wake wapo katika hali nzuri na shauku ya kuhakikisha wanafikia malengo kupitia mchezo huo muhimu.
Naye Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema maandalizi kwa ajili ya safari ya leo yamekamilika ingawa wanasikitika kuwaacha nyota wake watatu.
"Wachezaji wengine wote wapo katika hali nzuri na wataondoka kwenda kusaka alama tatu muhimu zaidi kwetu, tunahitaji ushindi ili kuendelea kuweka mazingira mazuri ya kucheza robo fainali, tunafahamu ugumu wa kundi letu lakini lazima tupambane mpaka mchezo mwisho," alisema Kamwe.
Yanga inashika nafasi ya tatu katika Kundi A ikiwa na pointi nne baada ya kucheza michezo minne, hivyo inahitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kutinga robo fainali ambayo kwa sasa wanaonekana kuigombania na MC Alger yenye pointi tano wakiwa nafasi ya pili nyuma ya Al Hilal.
Licha ya kucheza nje ya nyumbani, vigogo hao wa Sudan, Al Hilal wanaofundishwa na Mkongomani, Florent Ibenge, tayari wameshafuzu hatua ya robo fainali baada ya kufikisha pointi 10.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED