Samia atoa miezi mitatu waliokodishwa visiwa wakavitelekeza, kunyang'anywa

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 11:10 AM Jan 08 2025
Rais Samia Suluhu Hassan na Mwekezaji Andrea Azzola wakivuta kitambaa kuashiria ufunguzi wa hoteli iliyoko Kisiwa cha Bawe, Zanzibar jana, wakati wa shamrashamra za kuelekea miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
PICHA: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan na Mwekezaji Andrea Azzola wakivuta kitambaa kuashiria ufunguzi wa hoteli iliyoko Kisiwa cha Bawe, Zanzibar jana, wakati wa shamrashamra za kuelekea miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

RAIS Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, wametoa miezi mitatu kwa waliokodishiwa visiwa kufanya uwekezaji vinginevyo watapewa wengine.

Viongozi hao wamesema kuna wawekezaji wengine wanaohitaji visiwa hivyo kwa ajili ya kuweka miradi ya kiuchumi kwa maendeleo ya Zanzibar na taifa kwa ujumla.  

Wamesema visiwa hivyo vina faida kubwa katika uwekezaji na kila jambo jipya lina mambo yake kwa sababu serikali ya Zanzibar ilipotangaza kuwekeza katika visiwa, baadhi ya watu walikuwa wakali. 

Rais Samia na Dk. Mwinyi waliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa hoteli ya Bawe katika Kisiwa cha Bawe ambacho ni moja ya visiwa 15 vilivyokodishwa na serikali ya Zanzibar kwa ajili ya uwekezaji. 

Dk. Mwinyi alisema wawekezaji waliokodishwa visiwa na hadi sasa hawajafanya uwekezaji wowote, baada ya miezi mitatu, visiwa hivyo vitarejeshwa serikalini ili kupewa wengine wenye uwezo. 

Rais Samia alisema hivi sasa kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanyika hakuna anaejuta kwa sababu unakuza pato la taifa. 

Alisema amefarajika na uwekezaji wa visiwa vidogo na kuwapongeza wawekezaji pamoja na Mamlaka ya Kukuza Vitegauchumi Zanzibar (ZIPA) kusimamia kazi hiyo visiwani hapa.  

Samia alisema hiyo ni ishara tosha wawekezaji wanaridhika na kufanya uwekezaji ikizingatiwa kuwa sheria za uwekezaji zimefanyiwa marekebisho. 

Pia alisema katika uwekezaji huo, gharama zilizotumika ni Dola za Marekani milioni 42 ambazo si ndogo na kuna uwekezaji mkubwa umefanywa ukiwamo  kutengeneza umeme wa jua na kubadilisha maji ya chumvi kuwa maji safi kwa matumizi ya hoteli hiyo. 

Alisema Zanzibar ilikua na visiwa ambavyo vingekuza uchumi lakini uchumi ulikaliwa, hivyo kutumiwa na wavuvi pekee. 

Eneo hilo la kisiwa cha Bawe, limeleta manufaa makubwa ikiwamo ajira 400 kwa vijana na wawekezaji watalipa kodi kwa serikali na kupata mapato, hivyo kukuza jina la Zanzibar. 

Alisema mbali na maeneo mazuri ya uwekezaji, serikali imedhamiria kufanya mambo mengi ikiwamo uwekezaji katika bandari zikiwamo ya makontena ya Malindi, ya mizigo ya Fumba, Mpigaduri, Mkoani Pemba na bandari ya kushusha mafuta na gesi Mangapwani.

 Kwa mujibu wa Rais Samia, hayo yote yatakuza uchumi wa buluu na kupata maendeleo makubwa. 

Alisema katika jitihada za kuifungua Pemba kiuchumi, serikali inatarajia kujenga bandari kubwa ya abiria na mizigo Wete Pemba pamoja na bandari ya Kizimkazi, Kusini Unguja. 

Uwekezaji huo, alisema  utaimarika na juhudi za serikali kuimarisha viwanja vya ndege na wasafiri watavutiwa na huduma, hivyo aliwataka watendaji katika viwanja vya ndege kuongeza jitihada katika kutoa huduma. 

"Uwekezaji kufika visiwa ni jambo jipya kuendelea kuelimisha wananchi ili lisilete shida katika mahusiano," alisema na kuwataka watumiaji wa visiwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali na wawekezaji ili kuleta matokeo makubwa kwa maendeleo ya uchumi.  

Kuhusu Mapinduzi, alisema  yalilenga kuondoa ubaguzi na kustawisha maisha ya wananchi wa Zanzibar na hali zao. Alisema mapinduzi hayo yamewafanya wananchi kuishi kwa amani na kufanya shughuli zao za kijamii, kiuchumi na kimaendeleo. 

"Mapinduzi yametuletea neema. Nikiangalia  harusi za Zanzibar, nasema hii Zanzibar au Ulaya maana watu wanapendeza, wanatunzana mazawadi mbalimbali ya gharama," alisema.

 Rais Mwinyi kwa upande wake, alisema Rais Samia amekuwa msaada mkubwa kwa serikali ya Zanzibar katika mambo mbalimbali.

 Dk. Mwinyi alimpongeza mwekezaji wa kisiwa cha Bawe kuwa amefanya kazi nzuri kwa kuwa uwekezaji aliofanya ni wa kiwango cha kimataifa. 

Alisema wawekezaji wameendelea kuwasaidia wavuvi kwa ajili ya shughuli zao katika eneo hilo na samaki wanaowapata huwauza katika hoteli zilizomo kisiwani humo.  

Rais Dk. Mwinyi alizitaja faida za uwekezaji kuwa ni pamoja na ajira na kuwataka  Wazanzibari kusoma ili kuhudumu katika ajira kwenye sekta ya utalii. Faida nyingine ni kukua kwa masoko au bidhaa na kuongezeka kwa watalii.  

Waziri Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Sharif Ali Sharif, alisema uwekezaji huo ni historia ya kipekee kwa sababu mengi yaliyopita kupitia visiwa hivyo, faida yake imeonekana. 

Mkurugenzi Mkuu wa ZIPA, Saleh Saad, alisema mabadiliko na ukuaji na uwekezaji katika visiwa vya Zanzibar ni makubwa.  

Uzinduzi wa mradi huo wa hoteli ya Bawe ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.