Mwenyekiti kamati ya Miradi na Ufundi ya Bodi ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Ngwisa Mpembe ameipongeza Menejimenti ya RUWASA kwa kufanikisha utekelezaji wa miradi ambayo imewezesha mkoa wa Kilimanjari kufikia upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 84.5.
Amesema hatua hiyo inaifanya RUWASA kuwa na tumaini la kufika katika lengo la serikali ambalo ni huduma ya maji vijijini kufika asilimia 85 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025.
Pongezi hizo amezitoa akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa shughuli za wakala huo mkoani Kilimanjaro ambapo kamati hiyo imetembelea mradi wa maji wa Kikafu-Kwasadala-Bomang'ombe, pamoja na Jumuia ya watumia maji ya Uroki Bomang'ombe.
Awali akipokea taarifa ya maendeleo ya sekta ya maji vijijini, Meneja wa RUWASA mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Weransari Munis amesema huduma ya maji imefika asilimia 84.5 kwa mkoa lakini ipo miradi inayoendelea ambayo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2025 na itafikisha asilimia 89 ya huduma mkoani hapo.
Amesisitiza kuwa ndani ya miaka mitatu (3) ijayo huduma ya maji mkoani Kilimanjaro itakuwa asilimia 100 kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha fedha za miradi zinafikishwa katika maeneo husika.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Wolta Kirita amesema RUWASA inaendelea na jitihada mbalimbali ikiwemo kuhakikisha Dira za maji za Malipo Kabla ambazo tayari zimefanyiwa utafiti na kuonesha ufanisi zinatumika na kufungwa kila eneo la huduma ya maji nchini.
Ameihakikishia kamati kuwa lengo la serikali la huduma ya maji katika maeneo vijijini ambayo yanahudumiwa na RUWASA kufika asilimia 85 litanikishwa na ubora wa huduma utazingatiwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED