NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema pamoja na dunia kuweka mkazo, kwenye uzalishaji umeme kwa kutumia nishati jadidifu kama vile jua, maji na upepo, bado vyanzo vingine kama vile makaa ya mawe, vinahitajika kwa nchi za Afrika.
Dk. Biteko amesema hayo leo, Februari 11, 2025, New Delhi, India wakati akishiriki mjadala wa Mawaziri wa Sekta ya Nishati kutoka India, Qatar, Uingereza na Tanzania.
Mkutano huo ulikuwa na mada isemayo Mpango Mpya wa Dunia wa Biashara ya Nishati, ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa Wiki ya Nishati India.
Amesema Tanzania ina madini ya makaa ya mawe ya kutosha pamoja na urani, ambayo yanafaa kuzalisha umeme, hata hivyo kumekuwa na changamoto ya kupata ufadhili wa kuyaendeleza.
“Changomoto katika kuzalisha umeme yanatajwa kusababisha uchafuzi wa mazingira. Yanaweza kutumika kuzalisha umeme, kwa kutumia teknolojia ya kisasa yenye kuondoa sumu ya kaboni,” amesema Dk. Biteko.
Amesema kuwa takribani watu milioni 600 barani Afrika, hawajafikiwa na huduma ya umeme hivyo kwa kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali, ikiwamo makaa ya mawe itawezesha lengo la kufikishia umeme watu hao kwa haraka.
“Afrika inachangia uchafuzi wa mazingira kwa kiasi kidogo, kwa sababu ni bara maskini lakini inatajwa kuwa na mchango sawa na mataifa mengine, mabadiliko ya matumizi ya nishati hayakwepeki
“Nchi ziruhusiwe kuwa na uendelezaji endelevu wa rasilimali zake, kwa ajili ya kuwa na usalama wa nishati,” amesisitiza Dk. Biteko.
“Lazima tuangalie ukweli na hali halisi mfano Qatar au India hali yao ya upatikanaji umeme ni tofauti na Tanzania, hatutaweza kutumia njia ya aina moja kwa ajili ya kutatua changamoto za masuala ya umeme kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea ni lazima kutumia njia tofauti,”
Ameangazia lengo la Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi Afrika (Mission 300), uliofanyika nchini hivi karibuni wa kufikisha nishati ya umeme kwa watu milioni 300 barani humo, ifikapo mwaka 2030 na kusisitiza kuwa, Afrika inahitaji fedha na miundombinu ya kusafirisha umeme.
Waziri anayeshughulikia masuala ya Nishati kutoka Uingereza, Ed Milliband, ameipongeza Tanzania kwa mafanikio yake katika uzalishaji na usambazaji umeme kwa wananchi na hasa miradi katika nchi jirani.
Waziri wa Petroli na Gesi kutoka India, Hardeep Singh Puri, amesema mkutano huo unalenga kuwakutanisha pamoja viongozi wa sekta ya nishati, watunga sera na wavumbuzi kutoka maeneo mbalimbali duniani, ili kujadili changamoto zilizopo sekta hiyo na kutafuta suluhusho, kwa mustakabali endelevu wa upatikanaji wa nishati.
Aidha, mkutano huo utaangazia teknolojia za kisasa, mipango kabambe ya kupunguza uzalishaji kaboni na fursa za uwekezaji zinazoendana na malengo ya nishati kimataifa
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED