Bunge lataka ukarabati Uwanja wa Mkapa ukamilike Aprili 2025

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 05:21 PM Feb 11 2025
Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Picha:Mtandao
Uwanja wa Benjamin Mkapa.

BUNGE limeazimia mambo manne kuhusu Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwamo kuhakikisha ukarabati wake unakamilika ifikapo Aprili, 2025.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko ameyasema hayo leo bungeni alipokuwa akiwasilisha taarifa yam waka ya utekelezaji wa majukumu ya kamati hiyo.

Amesema serikali iandae mkakati wa kuanzisha chombo maalum cha usimamizi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa na viwanja vingine vinavyojengwa na Serikali ili kuhakikisha vinatunzwa na kuwa katika ubora wa kimataifa.

“Serikali iweke utaratibu wa sehemu ya makusanyo ya uwanja kubaki kwa matumizi ya uwanja huo ili kurahisisha matengenezo ya dharura yanapojitokeza  na iandae mkakati wa kuboresha viwanja vingine vya michezo ili kupunguza mzigo wa matumizi makubwa kwa Uwanja huo,”amesema.

Awali, amesema uwanja wa Benjamin Mkapa ni moja ya miundombinu muhimu ya michezo nchini inayotumiwa kwa matukio ya kitaifa na kimataifa, lakini unakabiliwa na changamoto za matengenezo na usimamizi endelevu.