Mwalimu auawa na mwenza wake, mtuhumiwa atoroka baada ya tukio

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 11:36 AM Feb 11 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase.

Jeshi la Polisi mkoani Pwani linamsaka Abdallah Mohamed (40), fundi friji mkazi wa Mataya, wilayani Bagamoyo, kwa tuhuma za kumuua mzazi mwenzake, Naomi Mwakajengele (28), mwalimu wa Shule ya Msingi Mataya.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Februari 10, wawili hao wakiwa chumbani kwao.

Kamanda Morcase alieleza kuwa majira ya saa nane usiku, majirani walisikia kelele kutoka kwa marehemu Naomi, akipiga yowe kwamba mwenza wake anamuua. Baada ya muda mfupi, Abdallah alitoka ndani na kuelekea chumba cha mfanyakazi wa ndani.

Inaelezwa kuwa Abdallah alimtaka mfanyakazi huyo kulala na watoto wawili wa marehemu, mmoja wa wiki moja na mwingine wa miaka minne, ambao awali walikuwa na mama yao.

Asubuhi, mfanyakazi wa ndani alishtuka baada ya jirani kuja kumuita Abdallah, huku akigundua kuwa mlango wa nyumba ulikuwa wazi na hakufahamu ni lini baba huyo wa familia aliondoka na kuelekea kusikojulikana.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mwili wa marehemu Naomi ulikuwa na majeraha yaliyosababishwa na kitu chenye ncha kali, maeneo ya ubavu wa kushoto na kulia, pamoja na kwenye chembe ya moyo.

Aidha, inadaiwa kuwa kabla ya tukio hilo, wawili hao walikuwa na migogoro ya ndoa iliyosababisha kutengana kwa muda mrefu, kabla ya Abdallah kurejea wiki mbili zilizopita, hali inayoaminika kuchangia tukio hilo la mauaji.

Kamanda Morcase ametoa wito kwa yeyote atakayemuona mtuhumiwa huyo kutoa taarifa katika kituo cha polisi kilicho karibu ili aweze kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.