RIPOTI MAALUM -2- Zinakotoka taka za plastiki zinazodhuru Ziwa Victoria

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:11 AM Feb 11 2025
Taka za plastiki zikisombwa na maji ya mto Mirongo, kuelekea Ziwa Victoria.
Picha:Mpigapicha Wetu
Taka za plastiki zikisombwa na maji ya mto Mirongo, kuelekea Ziwa Victoria.

SEHEMU ya kwanza ya ripoti hii jana iliangazia hatari ya kiafya inayovikabili viumbe katika Ziwa Victoria na watumiaji wa rasilimali zake kutokana na taka za plastiki zinazoingia ziwani, huku utafiti ukibaini kuwapo chembechembe za plastiki kwa asilimia 20 katika kila aina ya samaki (sato na sangara) wanaovuliwa ziwani. Mbali na samaki, ziwa hilo, lina mamba, viboko, kaa na mimea ya majini. Sasa endelea...

Kitogo Lawrance, Ofisa Mazingira kutoka Shirika la EMEDO mkoani Mwanza, anasema tatizo la taka za plastiki Ziwa Victoria halijatokea ghafla, bali ni matokeo ya tabia za binadamu, mifumo dhaifu ya udhibiti na ukosefu wa uwajibikaji wa pamoja. 

"Unajua plastiki Ziwa Victoria si jambo la bahati mbaya," anasema. "Haya ni matokeo ya mkusanyiko wa tabia mbovu za binadamu, udhaifu wa kisheria na kukosekana kwa hatua madhubuti."

Lawrance anabainisha kuwa kila kundi lina mchango wake katika tatizo hili. Wananchi wa kawaida mara nyingi hutupa taka za plastiki kiholela na wakati mwingine moja kwa moja ziwani, na mamlaka za serikali zimeshindwa kusimamia sheria kikamilifu. 

"Hata wavuvi wenyewe, kwa namna moja au nyingine, wanaweza kuchangia kwa kutupa mabaki ya vifaa vyao vya uvuvi," anasema Lawrance.

Mwongozo wa Udhibiti wa Taka Ngumu uliotolewa na serikali Septemba 2021, unabainisha chanzo kikuu cha taka za plastiki ni maeneo ya makazi, biashara, taasisi za elimu na watoa huduma za afya. 

Mwongozo huo unaelekeza kuwa, ikiwa maeneo haya yatatekeleza kanuni za kupunguza, kutumia tena na kurejeleza (3Rs), uwezekano wa taka za plastiki kuingia katika mazingira, likiwamo Ziwa Victoria, utapungua kwa kiasi kikubwa.

Lawrance anasema mito inayotokea maeneo ya miinuko na makazi ya watu husafirisha taka hizo hadi ziwani, akisisitiza changamoto kubwa ni udhaifu wa mifumo ya udhibiti. 

"Mfumo rasmi wa kudhibiti taka upo, lakini mara nyingi umeelemewa. Kwa hivyo, mito husomba taka ambazo hazikudhibitiwa vizuri kutoka katika makazi ya watu na hatimaye kuzifikisha ziwani," anasema.

Katika uchunguzi jijini Mwanza, mwandishi wa habari hii amebaini taka hizo hufika ziwani ama kwa kupelekwa na watumiaji wenyewe au kusombwa na maji ya mito mbalimbali ambayo huishia Ziwa Victoria. 

Mathalani kwenye Mto Mirongo, mwandishi aliona taka za plastiki zikiingia ziwani kupitia mto huo. Ni mto unaopita katikati ya maeneo ya makazi ya watu na sehemu za biashara katikati ya mji. Makopo, chupa za plastiki na taka nyingine hutupwa kiholela kando ya mto huo.

"Mvua ikinyesha, utajionea mwenyewe," anasema Mwajuma Chamndio, mkazi wa Mkuyuni, jijini Mwanza. "Mito yote hujaa taka kutoka huko milimani. Kwa mfano, ule mto mkubwa pale mjini (Mirongo), hujaa taka kibao, zikiwamo chupa na makopo. Yaani ni shida tupu."

Ofisa Mazingira wa Jiji la Mwanza, Fanuel Kasenene, anasema uelewa mdogo wa watumiaji bidhaa za plastiki ni moja ya vyanzo vikuu vya taka za plastiki Ziwa Victoria. 

Anasema wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu madhara ya plastiki kwa mazingira yao, hivyo wanaendelea kutupa taka ovyo, wakiona ni jambo la kawaida, bila kujua athari zake kwa mazingira na vyanzo vya maji.

"Elimu ndogo kwa wananchi juu ya madhara ya taka za plastiki huwafanya watu hawa kuendelea na tabia hizi, ambazo baadaye husababisha taka kuishia ziwani. 

"Matumizi ya plastiki yameenea hata kwa wavuvi na watumiaji wengine wa Ziwa Victoria, wakiwamo abiria wa vyombo vya usafiri wa majini, ambao mara nyingi hutumia bidhaa zilizowekwa kwenye vifungashio vya plastiki. Isivyo bahati, hakuna uhakika kwamba taka hizo zote hurudishwa nchi kavu baada ya matumizi.

"Kila siku unawaona wavuvi hapo wakielekea ziwani wakiwa na chakula kilichofungwa kwenye mifuko ya plastiki. Wengine hubeba soda, maji na vinywaji vingine vya kwenye chupa za plastiki. Kuna wavuvi wanaotumia mifuko fulani kujikinga na mvua, lakini uliwahi kuona wakirudi navyo baada ya safari yao?" anahoji Kasenene, akionesha jinsi plastiki zinavyoingia ziwani.

Wakati Kasenene akiwatupia lawama wananchi kuingiza taka ziwani, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Mwaka 2020/21 inabainisha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) hazifanyi kampeni madhubuti za uelimishaji jamii dhidi ya athari za uchafuzi wa mazingira utokanao na taka za plastiki katika maziwa makuu, bahari na utekelezaji sahihi wa mfumo wa R3 (kupunguza, kutumia tena na kurejeleza). 

Vifungu 17 na 18(2) vya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, vinaelekeza NEMC kusimamia na utekelezaji sheria za mazingira. Licha ya maelekezo hayo ya kisheria, uchafuzi wa mazingira unaendelea, hasa katika eneo hili la taka za plastiki Ziwa Victoria. Mikono ya waliopewa jukumu inaonekana kufa ganzi!

Robert Charles (42), mkazi wa Mkuyuni, jijini Mwanza anasema NEMC na mamlaka nyingine za serikali zingetimiza wajibu wake, uchafuzi wa mazingira unaoshuhudiwa Ziwa Victoria na kwingineko, usingekuwapo. 

"Ule uwajibikaji wa mamlaka za serikali ni mdogo sana," analalama Robert. "Hiki ndicho kinasababisha hizi taka kuenea ovyo. Taratibu zingezingatiwa na kusimamiwa vizuri, tatizo hili lingetatuliwa."

Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa, Jerome Kayombo, anakiri utekelezaji sheria za usimamizi wa taka za plastiki umekuwa ukisuasua, hata kusababisha changamoto kubwa ya uchafuzi wa Ziwa Victoria na kuathiri jamii inayotegemea ziwa hilo kwa maji na mahitaji mengine.

"Ukweli ni kwamba tatizo liko kwenye utekelezaji sheria," anasema Kayombo akitolea mfano wa sheria iliyopiga marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki nchini; kama ingetekelezwa kikamilifu, mifuko ya plastiki isingekuwapo tena ziwani. 

"Sheria ilizua kabisa matumizi ya mifuko ya plastiki. Kama hiyo sheria tungekuwa tunaitekeleza kama ilivyo, moja kwa moja tusingekuwa na mifuko ya plastiki kabisa," anasema.

Kayombo pia alisema sheria inawataka wazalishaji bidhaa za plastiki kuhakikisha taka zinazotokana na bidhaa zao baada ya matumizi zinakusanywa na kurejelezwa. 

"Sheria inamtaka mzalishaji bidhaa za plastiki kuhakikisha zile taka baada ya matumizi zinarudi, zinaokotwa kutoka kwenye mazingira na zinarejelezwa. Sasa kwa sababu hayo mambo hayafanyiki, taka zinarundikana kwenye mazingira na mvua ikinyesha, taka hizo husombwa na kuishia ziwani," anasema.

Katika hilo, Ofisa Mazingira wa Jiji la Mwanza, Kasenene, anakiri utekelezaji sheria na kanuni za usimamizi wa mazingira unakabiliwa na changamoto, hasa katika kuwashirikisha wamiliki wa viwanda.

Kasenene anaeleza kuwa utekelezaji mifumo ya uwajibikaji kwa wazalishaji wa plastiki unahitaji muda na bajeti, akisisitiza "si rahisi kufanikishwa kwa haraka".

"Unajua, kwa mfano, suala hili la kuwajibika kwa wazalishaji si kwamba halipo, lipo na wana mwitikio mzuri tu. Tumekuwa tunafanya nao vikao kadhaa, lakini utekelezaji ni wa polepole sana," anasema Kasenene. 

Anaongeza: "Hili si jambo la kuamkia usiku mmoja. Tunawaelimisha kwanza na kuhakikisha wanaelewa, ndipo wanajipanga na kuanzisha mifumo hiyo. Japo si rahisi sana, lakini tunajitahidi," anasema.

Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Taka Ngumu wa Mwaka 2018 unabainisha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya taka za plastiki zina uwezo wa kuchakatwa upya, lakini kiwango cha sasa cha urejelezaji ni chini ya asilimia 10.

Kwa kuzingatia takwimu hizo, Kasenene anasema kuna haja kuongeza nguvu katika utoaji elimu na usimamizi wa taka.

"Unajua wengi hatukuwa tunajua hatari za plastiki. Sisi (Jiji la Mwanza) tumekuwa tunafanya mikutano na wananchi ili waweze kupewa elimu juu ya hatari hizi. Tunaendelea na juhudi hizi ili angalau sehemu fulani ya jamii ikielewa, tutaweza kuwa katika nafasi nzuri ya kupambana na suala hili kwa undani wake," Kasenene anasema.