WIZARA ya Uchukuzi imesema kuwa faida iliyopatikana na uwepo wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ni kubwa kuliko hasara inayozungumzwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara akizungumza jana kuhusu uendeshaji wa ATCL, alisema serikali inachukua hatua madhubuti kuliimarisha, ikiwemo kuhamisha umiliki wa ndege kwenda ATCL jambo ambalo lipo kwenye hatua za mwisho.
Amebainisha kuwa manufaa yaliyopatikana kwa serikali kulifufua shirika hilo ni makubwa na ya kujivunia, kuliko hasara inayoelezwa.
Mathalani, amesema kwa hivi sasa ATCL inahudumia ndege 16 kulinganisha na umiliki wa ndege moja tu wakati ufufuaji ulipoanza.
Pia kwa kipindi chote cha mageuzi mpaka sasa ATCL imesafirisha abiria 5,670,631, kuingiza Sh. trilioni 1.88 na dola za Kimarekani milioni 410, fedha ambazo zina uwezo wa kununua ndegendogo za Bombadier 16 au Ndege za Airbus 7.
Mafanikio mengine kwa ATCL ni kujiendesha bila kuhitaji ruzuku ya kununua mafuta ya ndege au gharama ya matengenezo ya ndege au mishahara.
“Kwa muktahdha huo serikali inaliangalia Shirika kuwa na mchango mkubwa katika kuipeperusha bendera ya Tanzania, kuungaisha nchi yetu na mataifa mengine hususan nchi za Jumuiaya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), China na India,”amesema.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo ambaye kitaaluma ni mchumi amesema manufaa haya ni makubwa kuliko hasara inayozungumzwa mara nyingi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED