Madaktari bingwa wa macho kutoa matibabu bure Shinyanga

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 06:46 PM Jan 07 2025
news
Picha: Marco Maduhu
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Faustine Mlyutu.

Madaktari Bingwa wa Macho kutoka Hospitali ya Macho ya Dr.Agarwals tawi la Mwanza wanatarajia kutoa huduma ya matibabu ya macho bure kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga.

Huduma hiyo itatolewa siku moja tu, Ijumaa, Januari 9, 2025, katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Faustine Mlyutu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo, Januari 7, 2025. Mlyutu amesema kuwa wananchi wa Shinyanga wanapaswa kujiandikisha kuanzia Jumatano na Alhamisi (Jan 8-9) katika hospitali ya manispaa ili kupata fursa ya uchunguzi wa afya ya macho na matibabu bure siku ya Ijumaa.

"Madaktari hao ni wataalamu wa macho na wanapandikiza mboni ya jicho. Huu ni wakati mzuri kwa wananchi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kwa siku hizi mbili za kujiandikisha ili waweze kupata tiba," amesema Mlyutu.

Dk. Pierina Mwaluko, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, amesema kuwa ujio wa madaktari wa macho kutoka Dr.Agarwals ni fursa kubwa kwa wananchi wa Shinyanga kutatua matatizo ya macho, ambayo yamekuwa changamoto kubwa kwa baadhi yao.

1

Mratibu wa Huduma za Macho mkoani Shinyanga, Dk. Joseph Edward, amethibitisha kuwa tatizo la macho lipo mkoani humo, akiongeza kuwa kwa takwimu za miezi 10, watu 14,624 walikuwa na matatizo ya macho, na 1,213 walifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho.

Gandhi Babu, Mkuu wa hospitali hiyo tawi la Mwanza, amesema kuwa wao kama wataalamu wa matibabu ya macho wameguswa kutoa huduma bure kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa, kutokana na changamoto kubwa wanazokutana nazo katika huduma za macho.

"Katika huduma hii, tutapima matatizo ya uoni hafifu, presha ya macho, mtoto wa jicho, na pia tutatoa huduma ya kupandikiza mboni ya jicho kwa wale wanaohitaji," amesema Babu, akiwataka wananchi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya huduma hiyo ya bure.

2