CHAMA Cha ACT-Wazalendo kimesema kimefungua mashauri ya uchaguzi 51 ya kupinga matokeo na mwenendo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyika Novemba, mwaka jana.
Kwa mujibu wa taarifa yao iliyotolewa kwa umma na chama hicho jana, kesi hizo zimefunguliwa katika Mahakama za wilaya mbalimbali za Tanzania Bara na tayari hatua za awali ikiwamo wahusika kupokea wito wa mahakama kwa ajili ya kutajwa na kujibu mashauri zimeanza kufanyika.
Taarifa hiyo ilizitaja wilaya ambazo mashauri hayo yamefunguliwa kuwa ni Temeke, Lindi, Ilala, Momba, Mkuranga, Mafia, Kigoma na Kibiti.
“Chama cha ACT - Wazalendo kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kimejipanga kusimamia mashauri yote haya na tayari kimeshawapangia mawakili wake kesi watakazosimamia.
“Hatua ya kufungua mashauri haya ni mwendelezo wa dhamira ya chama kupigania demokrasia na haki za wananchi zilizoporwa wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, imani yetu kuwa kilichotokea kabla na siku ya uchaguzi hakikuwa uchaguzi bali uchafuzi na ahadi ya viongozi wetu ya kusimamia haki na demokrasia katika kila hatua,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliwataka wanachama na wapenzi wote wa demokrasia nchini kujitokeza kwa wingi wakati wa kesi hizo zinapoitwa mahakamani na chama kitaendelea kutoa taarifa ya kila hatua katika mwenendo wa mashauri hayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED