MAKUNDI ya WhatsApp yamesaidia kupatikana kwa ndugu wa Husna Shabani, aliyefariki dunia baada ya kupata ajali ya pikipiki Januari 4, 2025, maeneo ya Kwambonde, Wilaya ya Kibaha.
Husna, ambaye alikuwa akifanya kazi za kupika chakula kama kibarua eneo la Picha ya Ndege, hakuwa na taarifa kamili za mahali alipoishi wala mkoa alikotokea. Salim Manzi, mkazi wa Picha ya Ndege, ndiye aliyesambaza picha za Husna katika makundi mbalimbali ya WhatsApp ili kutafuta ndugu zake.
Akielezea tukio hilo, Salim alisema alipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuhusu ajali hiyo na walipofika mochwari, walithibitisha kifo cha Husna huku dereva wa bodaboda akidaiwa kujeruhiwa vibaya. “Tulitumia taarifa za marehemu alizoandika alipokuwa akitafuta kazi kwenye viwanda. Taarifa hizo zilionyesha sehemu alikotokea, na ndizo tulizotumia kuzisambaza kwenye makundi ya WhatsApp kutafuta ndugu zake,” alisema Salim.
Baada ya kusambaza taarifa hizo pamoja na picha, Salim alisema alianza kupokea simu kutoka kwa viongozi wa Halmashauri na Wilaya ya Uyui pamoja na ndugu waliothibitisha kumfahamu Husna. Mmoja wa ndugu wa Husna, Athumani Malengo, alisema alipokea taarifa hizo kutoka kwa baba yake kijijini Itobela, wakielezwa kuhusu ajali hiyo.
Athumani aliongeza kuwa kwa sasa wanaendelea na taratibu za kusafirisha mwili wa marehemu kwa ushirikiano wa ndugu na viongozi wa Wilaya ya Uyui. Selina Komba, mwajiri wa marehemu, alisema alikaa na Husna kwa mwezi mmoja lakini hakuwahi kufahamu kuhusu familia yake, kwani marehemu hakuwa wazi kuhusu mawasiliano ya ndugu zake.
“Alikuja kuomba kazi hapa kwangu akidai anaishi Picha ya Ndege, lakini hakuwahi kutuonyesha mahali hasa alipoishi. Nilipomuomba mawasiliano ya ndugu zake, hakutoa ushirikiano mpaka mauti yalipomkuta,” alisema Selina.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo. Alisema Husna alifariki dunia huku dereva wa bodaboda, Peter Benard, akijeruhiwa vibaya na anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi. Kamanda Morcase alisema ajali hiyo ilitokea baada ya dereva wa pikipiki aliyekuwa amembeba Husna kuingia barabarani bila kuchukua tahadhari na kugongwa na gari aina ya Nissan Kosta yenye namba za usajili T 180 DUP.
Kwa sasa, dereva wa bodaboda yupo katika chumba cha uangalizi maalum akiendelea na matibabu, huku dereva wa gari hiyo akishikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED