VITA ya madaraka ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), imeendelea kuvujisha siri yakiwamo yote ambayo yaliwahi kufanyika au kufanywa na viongozi wake kwenye vikao vyao vya ndani na vile vya nje ya chama hicho.
Tangu kuanza kwa vita hiyo, baada ya ‘vigogo’ wawili kutangaza nia ya kuwania nafasi ya uenyekiti taifa, siri za ndani ya chama hicho, zimekuwa zikitolewa kidogo kidogo kupitia kwa viongozi wenyewe katika mahojiano mbalimbali wanayofanya kwenye vyombo vya habari.
Vita hiyo pia, kwa takribani mwezi mmoja, imekuwa ikifanywa kwa njia mbalimbali ikiwamo kupitia mitandao ya kijamii, ikihusisha pande mbili za wafuasi wanaomuunga mkono Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wanaomuunga mkono, Tundu Lissu, ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara.
KAULI YA LISSU JANA
Jana Lissu akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akitokea nje ya nchi, alitoa siri nyingine ambayo alikuwa hajaisema hadharani.
Alisema kabla ya kutoka hadharani na kutangaza nia yake ya ‘kukitaka’ kiti cha uenyekiti, kulikuwa na mazungumzo mazito yaliyomhusisha yeye, Mbowe na viongozi wa dini kuhusu hatima ya nafasi mbili zinazotakiwa kugombewa ndani ya chama hicho.
Alisema mazungumzo hayo yalijikita kupanga nani awe Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa na nani awe mgombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Alisema wakati yeye (Lissu) na Mbowe walipokutanishwa kwenye mazungumzo hayo, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika alikuwapo.
Lissu alisema mazungumzo hayo yalifanyika kwa siku tatu mfululizo, hoja ikiwa ni kutafuta mwafaka katika kinyang`anyiro cha nafasi hizo mbili, ambazo viongozi hao wa dini walitaka wawili hao waamue.
Anaelezea zaidi kwamba yeye (Lissu), alifanya uamuzi wa kuwatamkia wazi viongozi hao wa dini kwamba anachotaka kugombea ni uenyekiti na kwamba kinyang`anyiro cha urais, anamwachia Mbowe.
Lissu alidai licha ya kueleza nia yake hiyo, lakini Mbowe kwa siku zote hizo tatu ambazo walikutanishwa, alieleza kwamba bado hajaamua chochote katika nafasi hizo zote mbili.
Kadhalika, Lissu alisema kuwa hata alipowaeleza wazi kuhusu nia yake hiyo, Mbowe hakukubaliana na uamuzi wake wa kutaka agombee nafasi hizo zote mbili, yaani uenyekiti na urais.
“Tulikutana kwa siku tatu, tukipatanishwa, tukizungumza juu ya hiki kinyang`anyiro na kwa siku tatu zote Mwenyekiti (Mbowe), alisema yeye hajaamua kugombea nafasi yoyote, Katibu Mkuu John Mnyika ni shahidi tukizungumza pamoja.
“Mwenyekiti hataki nitie nia, akiulizwa wewe...anasema mimi sijaamua, kwa siku tatu...nikaambiwa unasemaje, nikasema kwangu mimi suala la kuokoa hiki chama huko tunakoenda sio kuzuri, mimi niko tayari kugombea uenyekiti wa chama, urais nimwachie mwenyekiti, akakataa katakata (akimaamisha Mbowe),” alisema Lissu.
Lissu alisema baada ya mazungumzo hayo, hakuwahi tena kufanya mazungumzo yoyote na Mbowe.
“Kwa hiyo habari ya kusema mimi nataka yote, sijui siridhiki, si kitu chema kusema mwenyekiti amedanganya, lakini kwenye hili amedanganya,” alisema Lissu.
“Amekataa nisigombee uenyekiti, amekataa nisigombee urais wakati yeye anasema hajaamua, eti anasema inabidi tuangalie kwanza, tupime upepo ila yeye hayuko tayari...kwa siku tatu,” alisema.
Alisema walitakiwa kuzungumza na viongozi wa dini watatu, lakini walifanikiwa kuzungumza na kiongozi wa dini mmoja pekee.
“Nasikia huko wanasema huyo alipelekwa kwa viongozi wa dini...ni kwamba niliitwa na viongozi wa kidini watatu na nimekutana na mmoja tu...kwanza nilipokubali tu kukutana nao, Mwenyekiti ‘aka-loose interest (akakosa hamu ya kuendelea),” alisema Lissu.
“Niliwekewa mgombea kwenye nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, nikasaema aaaa…mimi nishindane na Ezekiel Wenje, ni bora nishindane na aliyemtuma.”
Akizungumzia kuhusu hatua ya John Heche kutangaza kuwa upande wake, Lissu alisema anamtambua kama miongoni mwa wanachama ambao ni hazina kwa chama hicho.
Pia, alisema Heche ndiye alisababisha wao wakafahamu mambo mengi ambayo yalijadiliwa katika vikao vya maridhiano kati ya viongozi wa chama hicho na serikali.
“Heche ni moja ya hazina kubwa ya chama chetu, amekuwa mbunge wa chama chetu, amekuwa Mwenyekiti wa BAVICHA na Mjumbe wa Kamati Kuu. Sasa mimi nizungumzie nafasi yake ya Kamati Kuu na ubunge ambako nimefanya naye kazi kwa karibu.
“Heche alikuwa kwenye Kamati ya Maridhiano kama alivyosema, kama asingekuwa kwenye kamati hiyo ya maridhiano, tusingejua mambo mengi sana, kwa hiyo tutakapoandika historia sawa sawa ya haya maridhiano, tutamshukuru kwa kuwa, kwa sababu yake tulijua mambo mengi sana.”
MINYUKANO ILIVYOANZA
Vita ya madaraka kati ya kundi la Mbowe na Lissu, iliyoanza kama minyukano kwenye mitandao ya kijamii, ambako siri za CHADEMA zilianza kuvujishwa na wanachama na wafuasi wa vigogo hao, lakini baadaye vigogo hao kwa nyakati tofauti wametoka hadharani na kueleza kile kinachoendelea.
Minyukano hiyo imekwishawaibua viongozi waandamizi, wakiwamo wagombea wa nafasi za uongozi kwenye uchaguzi uliopangwa kufanyika Januari 21, mwaka huu, katika ukumbi wa Mlimani City, mkoani Dar es Salaam.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Victoria, Wenje, ambaye anagombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, alitangaza kumuunga mkono Mbowe.
Mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Heche, naye amejitokeza na kutangaza kumuunga mkono Lissu kwenye uchaguzi huo.
Heche na Wenje, wamekuwa wabunge kwa nyakati tofauti katika majimbo ya Tarime na Nyamagana, mtawalia.
Makada hao wote ni wajumbe wa Kamati Kuu na Mkutano Mkuu utakaochagua viongozi wakuu wa chama.
Kabla ya wanaowaunga mkono, Lissu kama mgombea katika nafasi hiyo ambayo imezua vita kali, ndiye alianza kwa kutoa mbele ya kamera kutoa baadhi ya siri au mambo yaliyokuwa yakiendelea ndani ya chama chake huku wenzake (Mbowe), akinyamaza kwa muda.
Hata hivyo, baadaye Mbowe naye alitoka hadharani na kuzungumza kidogo wakati akihojiwa hivi karibuni.
Katika mkutano wake baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti bara, Heche alisema kwamba anamuunga mkono Lissu kugombea nafasi hiyo kutokana na mrengo wake wa kutaka haki, ukweli na uwazi ndani ya chama hicho, huku akisema ataendelea kumtambua na kumheshimu Mbowe kama baba yake na mlezi wake kisiasa.
Uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama hicho, unatarajia kufanyika Januari 21, mwaka huu na dirisha la kuchukua fomu kwa wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo lilifungwa juzi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED