STRAIKA Erick Okutu wa Pamba Jiji, amekataa mpango wa kupelekwa KenGold kwa mkopo akisema ni bora avunje mkataba wake wa miezi sita uliobaki kuliko kupelekwa timu asiyoitaka.
Okutu, raia wa Ghana, amesema hayo kutokana na tetesi kuwa atatolewa kwa mkopo kwenye Klabu ya KenGold katika kipindi chake cha mkataba uliobaki.
Alisema hana taarifa yoyote ya kwenda KenGold, akisema yeye anafahamu kuwa ni mchezaji halali wa Pamba Jiji.
"Sina taarifa juu ya kutolewa kwa mkopo kwani ninachofahamu bado nina mkataba wa miezi sita na kikosi hiki, sina mpango wowote wa kuondoka, labda itokee ofa kutoka nje ya nchi," alisema.
Imeelezwa kuwa viongozi wa Pamba wanahitaji kumpeleka Okutu kwa mkopo KenGold baada ya kumsajili mshambuliaji raia wa Mkenya, Mathew Tegisi Momanyi, kutoka Shabana FC ya nchi humo.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Pamba, Ezekiel Ntibikeha, alisema masuala ya usajili na kila kitu kinachoendelea kitawekwa hadharani muda utakapowadia na sasa wanachofanya ni kazi ya kuboresha kikosi.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema sababu za nyota huyo kutaka kutolewa ni kutokana na kukorofishana na kocha wa timu hiyo, Fred Felix ‘Minziro’, alipojibizana naye kutokana na kuoneshwa kadi nyekundu katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Prisons Desemba 26, mwaka jana.
Nyota huyo alijiunga na timu hiyo msimu huu baada ya kuachana na Tabora United aliyojiunga nayo mara ya kwanza msimu wa 2023.24, akitoka Hearts of Lions ya Ghana. Msimu uliopita alipachika mabao saba kwenye Ligi Kuu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED