KIKOSI cha Yanga kinatarajia kuondoka saa 10:00 alfajiri ya kuamkia kesho kuelekea nchini Mauritania kwa ajili ya mchezo wa raundi ya tano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa nchini Mauritania Jumapili ijayo saa 4:00 usiku kwenye Uwanja wa De la Capitale, jijini Nouakchott, huku Yanga itashuka dimbani katika mechi hiyo kwa tahadhari kubwa, ikitangaza pia urejeo wa kiungo mshambuliaji wao, Clatous Chama.
Al Hilal inacheza mechi zake nchini humo kutokana na kuwapo kwa machafuko ya kisiasa nchini Sudan.
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema inabidi waende nchini huko kwa tahadhari na kucheza mechi kwa mahesabu makubwa kutokana na ugumu na umuhimu wa mchezo huo ambao kwao hauhitaji chochote zaidi ya ushindi.
"Tunakwenda huko kwa ajili ya kusaka pointi tatu tu na si vinginevyo, tutakwenda kucheza kwa tahadhari kubwa kulingana na ubora wa mpinzani wetu, hatutakwenda kufunguka sana kwa sababu Al Hilal ni timu yenye ubora zaidi linapokuja suala la mashambulizi ya kushtukiza, ni mechi ngumu ambayo inabidi twende kucheza kwa mahesabu makali kwani hatuna tunachohitaji zaidi ya ushindi, tukipata pointi tatu basi tutakuwa na matumaini kwa sababu mechi yetu ya mwisho dhidi ya MC Alger tutacheza tukiwa nyumbani," alisema Kamwe.
Kamwe, pia aliwapa habari nzuri kwa wanachama na mashabiki wa Yanga kwa urejeo wa mchezaji Clatous Chama ambaye kwa muda mrefu hakuwa uwanjani kutokana na kukabiliwa na majeraha.
"Wachezaji wako vizuri na Chama amepona, amerejea kwenye kikosi na atakuwa mmoja kati ya watakaosafiri, ila Yao Kouassi ndiyo bado majeruhi, hatakuwapo kwenye kikosi," alisema.
Yanga ambayo ilipoteza mechi zake mbili za kwanza, kwa mabao 2-0 dhidi ya Al Hilal na MC Alger, lakini ilikuja kuzinduka na kuzoa pointi zote nne kwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambapo ilipata sare ya bao 1-1 ugenini na kuifunga mabao 3-1 nchini.
Kwa sasa ipo nafasi ya tatu ya masimamo wa Kundi A, ikiwa na pointi nne, hivyo inahitaji ushindi kwenye mchezo wa Jumapili ili kufikisha pointi saba.
Yanga inakwenda kucheza na timu ambayo tayari imeshafuzu hatua ya robo fainali ikifikisha pointi 10, lakini wenyeji bado wanahitaji ushindi ili kumaliza kinara wa kundi kwa ajili ya kupata faida mbele ya safari kwa kucheza na mshindi wa pili wa makundi mengine, pia kuanzia ugenini mechi za robo fainali na kumalizia nyumbani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED