Mpepo kurejea Ligi Kuu Bara

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 08:55 AM Jan 08 2025
Eliuter Mpepo.
Picha: Mtandao
Eliuter Mpepo.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Tanzania Prisons na Geita Gold, Eliuter Mpepo, huenda akaonekana tena kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu Bara baada ya klabu mbili kuingia vitani kusaka saini yake.

Mpepo ambaye alikuwa akicheza Ligi Kuu ya Zambia, inaelezwa yupo kwenye mazungumzo na Klabu ya Tabora United huku pia Kengold FC nao wakitajwa kuhitaji huduma ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Taarifa kutoka ndani ya Klabu ya Tabora United zinaeleza kuwa mazungumzo yao na Mpepo yanaenda vizuri na huenda wakamtangaza kuwa mchezaji wao kabla ya dirisha dogo kufungwa.

"Bado hatujafikia muafaka, lakini tupo kwenye mazungumzo kuangalia uwezekano wa kumsajili ya kukiongezea nguvu kikosi chetu kwa ajili ya mzunguko wa pili," alisema mmoja wa viongozi wa klabu hiyo.  

Kiongozi huyo alisema Mpepo wameona ni mchezaji muafaka wa kuongeza nguvu kwenye safu yao ya ushambuliaji kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.

Mbali na Tabora United, nyota huyo pia anawaniwa na Kengold na Tanzania Prisons aliyoichezea huko nyuma na kutoa mchango mkubwa.

Mpepo alijiunga na Klabu ya Trident akitokea Mtibwa Sugar msimu wa 2023/2024, lakini kwa sasa nyota huyo ameachana na timu hiyo.