Serikali yatafuta mwarobaini walimu kutumia vifaa vya maabara kwa ufanisi

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 05:43 PM Jan 07 2025
Baadhi ya walimu wa somo la Fizikia wakitengeneza mifumo ya umeme, wakati wa mafunzo ya vitendo yanayoendelea katika Shule ya Sekondari Tarime, mkoani Mara.
Picha: Grace Mwakalinga
Baadhi ya walimu wa somo la Fizikia wakitengeneza mifumo ya umeme, wakati wa mafunzo ya vitendo yanayoendelea katika Shule ya Sekondari Tarime, mkoani Mara.

IMEBAINISHWA kuwa, baadhi ya walimu wanaofundisha masomo ya Sayansi katika shule za sekondari, wanakosa ufanisi katika kutumia vyema vifaa vya maabara, hali inayochangia kupunguza ari kwa wanafunzi kupenda kusoma masomo hayo wakidai ni magumu.

Hayo yamesema leo na Mkufunzi wa Somo la Fikizia kutoka Chuo cha Ualimu Mkoa wa Morogoro, Felix Nestory ambaye ni mwezeshaji wa Mafunzo kwa Walimu wa Masomo ya Sayansi, Hisabati na Tehama kutoka mikoa ya Simiyu na Mara yanayofanyika wilayani Tarime.

Mkufunzi Nestory ameeleza kuwa  jambo  hilo, linaathiri kwa kiasi kikubwa ubora wa ufundishaji wa masomo ya Sayansi kwa sababu  yanajikita zaidi kwenye nadharia badala ya mazoezi ya vitendo.

Matumizi sahihi ya vifaa vya maabara ni muhimu kwa wanafunzi kwa sababu yanawezesha kuelewa dhana za sayansi kwa njia ya vitendo, vifaa vya maabara ni nyenzo zinazosaidia wanafunzi kuona mifano halisi ya kinachoelezwa kwenye nadharia, kama vile mchakato wa kemikali, majaribio ya kimwili, au michakato ya biolojia,” alisema Nestory.

Amesema katika kutatua changamoto hiyo, tayari Serikali imeanza kutoa mafunzo kwa walimu wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Tehama kuwajengea uwezo wa kuboresha mbinu za ufundishaji na kuongeza  katika kutumia vifaa vya maabara kwa ufanisi.

Mratibu wa Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP), Dk.  Nicholaus Gati, amesema kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatoa mafunzo maalum kwa walimu wa masomo ya Sayansi, Hisabati, na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji.

Amesema  mafunzo hayo yanatolewa kwa lengo la kuboresha ufanisi wa walimu na kuhamasisha matumizi bora ya vifaa vya maabara, teknolojia, na mbinu za kisasa katika ufundishaji wa masomo.

“ Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za Wizara kuhakikisha kuwa walimu wanapata ujuzi na rasilimali muhimu zinazohitajika ili kutoa elimu bora na yenye tija kwa wanafunzi, tumedhamiria kuondoa changamoto zinazozikumba shule za sekondari, hasa katika matumizi ya vifaa  vya  teknolojia, ili wanafunzi waweze kuelewa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa vitendo, badala ya kuendelea kuyakimbia kwa kuwaona kuwa ni magumu,” amesema Dk. Gati.

Mwalimu wa somo la Hisabati, katika Shule ya Sekondari Kishamapanda iliyopo Halmashauri ya Busega, Piencia Mugizi, amesema mbinu  za ufundishaji walizofundishwa  zitawasaidia  wanafunzi  kuona masomo ya Sayansi  ni rahisi kwa sababu wanajifunzi kwa vitendo.