MIAKA 61 YA MAPINDUZI: Dk. Mwinyi ajivunia maendeleo katika elimu na uchumi wa bluu

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 11:29 AM Jan 06 2025
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akiondoa pazia kuweka Jiwe la Msingi la Ufunguzi wa Skuli ya Sekondari Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja, ufunguzi huo.
Picha: Mtandao
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akiondoa pazia kuweka Jiwe la Msingi la Ufunguzi wa Skuli ya Sekondari Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja, ufunguzi huo.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar imepata maendeleo kila sekta, ikiwamo ya elimu katika miaka 61 ya mapinduzi.

Alisema hayo wakati akiweka jiwe la msingi jengo la utawala na taaluma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam - Taasisi ya Sayansi za Bahari huko Buyu, nje ya mji wa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alisema sera kuu ya uchumi katika serikali yake ni uchumi wa buluu na katika sekta hilo kuna utalii ambao unachangia pato la taifa kwa asilimia 30.

Alitaja sekta zingime ni uvuvi, kilimo cha mwani na mazao ya baharini, hivyo chuo hicho ni muhimu na nchi itapata wataalam wa uvuvi na mazao ya bahari.

Alisema sekta nyingine ni bandari, mafuta na gesi, usafiri na uzalishaji baharini, hivyo taasisi ya chuo hicho ni muhimu na itatoa wataalam wa uchumi wa buluu.

Rais Dk. Mwinyi alisema matarajio kuwa chuo kitatumia utafiti mbalimbali wa uchumi wa buluu na wataalam watakaotoka hapo wataleta utafiti huo na kusaidia kupata maendeleo.

Mkuu wa Chuo hicho, Dk. Jakaya Kikwete alisema kuwa bila uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mradi wa HIT unaofandhiliwa na Benki ya Dunia, shughuli hiyo isingefanyika na kwa uamuzi huo anastahili kupongezwa kwa kuwa haikuwa rahisi kushajiisha taasisi hiyo kwenye mradi huo.

Alisema isingeweza kufanya ujenzi huo bila kuwa na hatimiliki ya ardhi ya eneo la chuo hicho ambayo ni moja ya masharti ya Benki ya Dunia na kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kukipatia chuo hati hatimiliki ya ardhi katika eneo hilo na kukamilisha ujenzi wa barabara katika eneo hilo.

Kikwete, Rais wa Tanzania wa Awamu ya Nne, alisema hatua hiyo imerahisisha usafiri kwa wanafunzi na wafanyakazi na kusema kuwa Dk. Mwinyi hana mbadala wake katika utekelezaji ahadi zake za maendeleo.

Alisema kasi ya maendeleo Zanzibar ni kubwa na maendeleo yanafanyika. Zanzibar ya zamani si sawa na ya sasa.

Waziri wa Uchumi wa Buluu, Shabani Othman alisema kwenye sera ya uchumi wa buluu, kuna vipaumbele vitano, ikiwamo uvuvi na ukulima wa mwani ikijumuisha mazao ya baharini.

Alisema ili kutimiza malengo katika vipaumbele hivyo, kunahitajika rasilimali watu, utafiti na teknolojia na utalamu, vyote hivi sasa vipo katika chuo hicho, hivyo wizara yake itatoa ushirikiano kwa chuo.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhammed Mussa, alisema katika kufanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya elimu, serikali imewekeza katika uchumi wa buluu na Zanzibar lazima izae matunda. Wizara yake imeandaa mitaala ambayo itatoa wanafunzi wenye sifa watakaojiunga katika chuo hicho.

Alisema wizara itahakikisha inawajengea wanafunzi ujuzi wa ziada ili kutoa mabaharia wengi na watalamu wa uvuvi ambao watatumia vifaa vya kisasa katika kuvua.

Waziri wa Elimu na Sayansi, Prof. Adolf Mkenda, alisema bila mapinduzi, mageuzi ya elimu yasingeweza kufikiwa.

Alimpomgeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuhakikisha hakuna mkwamo katika ujenzi huo na kupongeza serikali kwa uamuzi wa kuazisha Chuo cha Teknolojia ya ICT na kampasi ya chuo hicho ya kimataifa kuazishwa Zanzibar.

"Tunachofanya leo ni sehemu tu ya miradi ambapo Serikali ya Tanzania ilichukua mkopo Benki ya Dunia kuimarisha elimu ya chuo kikuu na taasisi za elimu ya juu Tanzania ili kutawanya fursa ya elimu ya juu," alisema.

Waziri Mkenda alisema chuo hicho kimepata mgawo wa fedha hizo Sh. bilioni  34.6 na kuvitaka vyuo vikuu kutoa shahada zinazoendana na mageuzi ya elimu.

Akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu mradi huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Prof. Willium Anangisye, alisema mradi huo ni uwekezaji unaofanyika kwa lengo la kuzalisha maarifa ya kuimarisha taaluma ndani na nje ya nchi kiuchumi, kijamii na kiteknolojia. 

Alisema hiyo pia ni mkakati wa chuo kuzalisha maarifa, utafiti na kuimarisha mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia kwa wanafunzi na wafanyakazi. 

Alisema mradi huo unatekelezwa na serikali kupitia Wizara ya Sayansi na Teknolojia kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kwa lengo la kuimarisha elimu ya vyuo vikuu nchini, kikiwamo Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewapatia hekta 50.24 katika eneo la Buyu ambako ndiko kiliko chuo hicho. Ujenzi wa mradi huo ulianza mwaka 2022 na hadi kukamilika kwake utagharimu jumla ya Sh. bilioni 11.1 na utakamilika Agosti mwaka huu.

Alisema kuwa mradi huo utakapokamilika, utaleta mabadiliko makubwa ikiwamo kuongezeka kwa wanafunzi kutoka 140 hadi 300, kuongeza fursa ya kuambatanisha wanataaluma katika kampuni za kazi na kutembelewa na wanataaluma waliobobea ili kubadilishana uzoefu kwa wanafunzi, kuongeza ubora wa ufundishaji na ufunzaji na kuongeza soko la ajira kwa ujumla.

Alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa mafanikio makubwa katika miaka ya uongozi wake ambayo yamefanyika kwa ufanisi mkubwa na yamejionesha katika uimarishaji uchumi, miundombinu, ukusanyaji mapato na kusimamia matumizi ya fedha za umma.