MBUNGE wa Jimbo la Mpanda mjini, Sebastian Kapufi amewataka watendaji wa serikali wapoandaa taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo wasiishie kumshukuru Rais pekee kwa kupeleka fedha za miradi hiyo bali wamkumbuke na yeye.
Alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo aliyoifanya katika kata zilizopo kwenye Jimbo la Mpanda mjini.
"Mwalimu nashukuru tunamshukuru Mama Samia...kwa kutuletea fedha, ukimshukuru hata na mbunge wala hukosei kwa kuwa ndio napiga kelele kwenye Bunge kule bajeti ije huku.
Kwa hiyo mnapoandika haya mavitu msisahau kutaja na hilo...kwa hiyo bila sisi kukaa kule kupitisha bajeti hamuioni mia huku...kwa hiyo ni mchakato," alisema.
Alisema anapeleka shukrani kwa kila mmoja kutokana na jitihada zake ndio maana miradi inakamilika na manufaa yanaonekana kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu.
Kauli ya Mbunge Kapufi imekuja baada ya kuona katika maeneo mengi, kama ilivyo Shule ya Sekondari Kapalakangao iliyopo Kata ya Kazima kukagua miradi ya maendeleo jitihada zake hazitajwi.
Awali, katika Shule ya Sekondari Kapalakangao, Mkuu wa shule hiyo, Mario Mhagama katika taarifa yake ya utekelezaji wa mradi wa nyumba pacha za walimu walipokea zaidi ya Sh. milioni 110.
Alisema katika shule kuna changamoto kadhaa ikiwamo ya upungufu wa walimu na ukosefu wa nishati ya umeme na walimwomba mbunge awasaidie, lakini hawakutambua mchango wake wa kupigania maendeleo ya kielimu katika jimbo hilo.
Mbunge huyo alichangia Shilingi milioni saba kutoka mfuko wa jimbo ikiwa ni kwa ajili ya kutatua changamoto ya ukosefu wa nishati ya umeme.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED