Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, ameonesha kuridhishwa na kasi ya kilimo cha pamba wilayani Kishapu, akisema kuwa zao hilo linarejea kwenye heshima yake kama mkombozi wa wakulima kiuchumi.
Akiwa katika ziara ya kutembelea mashamba ya wakulima wa pamba jana, RC Macha alisema kuwa mwenendo wa kilimo cha zao hilo umeimarika, na juhudi zinazofanywa na wakulima zinaendana na mkakati wa serikali wa kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
"Nimefuatilia na kukagua mashamba yenu, na niseme kuwa nimeridhishwa sana na kasi ya kilimo cha pamba hapa Kishapu. Hakika sasa tunakwenda kurejesha heshima ya zao la pamba kama ilivyokuwa awali. Hili ndilo kusudio la Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kilimo cha pamba kinakuwa na tija kwa mkulima, kuchochea uchumi wa wananchi na kuongeza pato la Taifa," amesema RC Macha.
Aidha, amewataka wataalamu wa kilimo kuhakikisha wanaendelea kuwafikia wakulima mashambani kwa kuwapatia elimu ya kilimo chenye tija. Alisisitiza pia matumizi ya teknolojia kama vile ndege zisizo na rubani (drones) kunyunyizia dawa kwa ufanisi ili kuimarisha uzalishaji wa pamba.
RC Macha amebainisha kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kila mkulima anavuna kati ya kilo 1,000 hadi 1,200 kwa hekari moja, badala ya kiwango cha sasa cha kilo 100 hadi 300 ambacho kinamkwamisha mkulima kiuchumi.
Baadhi ya wakulima waliotembelewa na Mkuu wa Mkoa wameishukuru serikali kwa kuwapatia elimu ya kilimo bora na kuwaunga mkono kwa kuwafikia mashambani kwa vitendo. Walisema kuwa kwa sasa wana matumaini makubwa ya kuinuka kiuchumi kupitia kilimo cha pamba.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED