Hasunga aliamsha bungeni madai fidia, serikali yafafanua

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 06:17 PM Feb 14 2025
Japhet Hasunga Mbunge wa Vwawa (CCM).
Picha: Mtandao
Japhet Hasunga Mbunge wa Vwawa (CCM).

Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, amesema serikali ipo katika hatua za mwisho za kuwalipa fidia wananchi wa Iboya, Kata ya Ihanda, mkoani Mbeya ili kuruhusu ujenzi wa barabara utakaosaidia kupunguza msongamano wa magari.

Ametoa ufafanuzi huo leo, Februari 14, 2025, bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga, aliyekuwa akitaka kufahamu lini wananchi wa eneo hilo watalipwa fidia baada ya kupisha ujenzi wa barabara.

Kasekenya amesema serikali inatambua kuwa wakazi wa Iboya wanadai fidia ya Shilingi bilioni 4.9 na kwamba hatua za malipo zipo katika hatua za mwisho.

“Tunavyoongea sasa, Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha zipo katika hatua za mwisho za kuwalipa fidia wananchi ili kituo hicho kijengwe na kupunguza msongamano wa magari Tunduma,” amesema Kasekenya.