Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuhutubia na kulivunja rasmi Bunge la 12 Juni 27, 2025.
Akitoa taarifa ya Spika bungeni Leo kuhusu matukio muhimu kuelekea mkutano wa 19, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, amesema Rais atahutubia baada ya Waziri Mkuu kutoa hotuba ya kuhitimisha shughuli za Bunge la 12, Juni 26, 2025.
Zungu amesema Aprili 8, 2025 Mkutano wa Bajeti utaanza rasmi na Bajeti ya serikali itasomwa Juni 12, 2025.
Awali, alieleza kuwa Machi 10, 2025 vikao vya Kamati za kudumu za bunge zitaanza na serikali itawasilisha kwa Katibu wa Bunge nakala za dondoo za vitabu vya bajeti pamoja na randama za makadirio hayo kwa Mwaka wa fedha wa 2025/26 kwa mujibu wa kanuni.
“Machi 15, 2025 utafanyika mkutano wa wabunge wote ambapo Waziri wa Mipango na Uwekezaji atawasilisha mapendekezo ya Mpango wa fedha wa 2025/26 na Waziri wa Fedha atawasilisha mapendekezo ya serikali ya bajeti, kiwango na ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2025/26,”amesema.
Amesema Machi 12, 2025 kamati za kudumu za kisekta zitaanza ziara za kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi iliyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha ulioisha Juni 30, 2025.
“Machi 19, 2025 Kamati za kudumu za kisekta zitaanza uchambuzi wa taarifa za utekelezaji wa bajeti za wizara zinazosimamiwa na kamati hizo na Aprili 2, 2025 vikao vya mashauriano kati ya kamati ya uongozi, kamati ya bajeti na serikali vitaanza kufikiria masuala mbalimbali yaliyojitokeza wakati zikijadili utekelezaji wa kazi za Wizara,”amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED