Mapango ya Amboni kuboreshwa kuvutia watalii

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 08:08 PM Feb 14 2025
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Ngorongoro, Makao Makuu, Mariam Kobelo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Ngorongoro, Makao Makuu, Mariam Kobelo.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imepanga kufanya maboresho makubwa katika Hifadhi ya Mapango ya Amboni, jijini Tanga, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi. Hatua hii inalenga kuchangia ongezeko la mapato yatokanayo na sekta ya utalii na kuimarisha pato la Taifa.

Kwa mwaka 2024, takriban watalii 13,000 walitembelea Mapango ya Amboni, lakini Mamlaka ina lengo la kuongeza idadi hiyo ili kuhakikisha mapango hayo yanazidi kuwa kivutio kikubwa cha utalii.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Ngorongoro, Makao Makuu, Mariam Kobelo, amebainisha hayo leo wakati wa hafla ya Diko la Amboni, iliyoandaliwa na Mamlaka hiyo, ambapo wapishi watano walishindanishwa katika maandalizi ya vyakula mbalimbali.

"Sekta ya utalii inahusisha mambo mengi, na kuna mipango madhubuti kuhakikisha Mapango ya Amboni yanakuwa salama na ya kuvutia kwa wageni. Tunataka mtalii anapokuja hapa afurahie uzuri wa eneo hili," alisema Kobelo.

Amefafanua kuwa maboresho hayo yanajumuisha uboreshaji wa miundombinu, ikiwa ni pamoja na:

Kuboresha geti la kuingilia ili kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unakuwa wa uhakika na salama.
Kuboresha mandhari ya mapango kwa kuweka maeneo ya kupumzikia kwa wageni.
Kuanzisha maeneo ya kambi kwa ajili ya watalii wanaotaka kufurahia mazingira ya mapango kwa muda mrefu.