Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, Korir Sing’oei, ameipuuzilia mbali barua kutoka kwa Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) inayomuunga mkono Richard Randriamandrato wa Madagascar katika kinyang’anyiro cha Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Akizungumza mjini Addis Ababa leo Ijumaa, Februari 14, Sing’oei amesisitiza kuwa Kenya itaendelea kusimamia azma yake ya kumfanya Raila Odinga kuwa mwenyekiti wa AUC, huku kampeni zake zikilenga kushirikisha tena nchi wanachama wa SADC.
Aidha, ametilia shaka ugombea wa Madagascar, akieleza kuwa kijiografia, taifa hilo lina mfungamano mkubwa na Kusini mwa Afrika kuliko Afrika Mashariki.
"Ni muhimu kutambua kuwa ni zamu ya nchi kutoka Kanda ya Mashariki kushika nafasi ya uenyekiti wa AUC. Madagascar ni nchi yenye hali ya kipekee kwa kuwa inapakana na kanda zote mbili—Mashariki na Kusini. Ikiwa ingekuwa zamu ya Kusini mwa Afrika, bado inaweza kuwasimamisha wagombea wake, jambo linaloiweka katika nafasi ya upendeleo usio wa haki," amesema Sing’oei.
Jana, SADC iliandikia nchi wanachama wake 16 kuomba uungwaji mkono kwa Madagascar ili imrithi mwenyekiti wa sasa wa AUC, Moussa Faki.
Mbali na Richard Randriamandrato wa Madagascar, kinyang’anyiro hicho kinajumuisha pia Raila Odinga wa Kenya na Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Mahamoud Ali Youssouf.
Kwa sasa, Odinga ndiye mgombea pekee kutoka Afrika Mashariki, huku Madagascar ikiwa mgombea wa pekee wa SADC baada ya Mauritius kujiondoa.
Uamuzi wa SADC unafuata makubaliano ya mkutano wa Baraza la Umoja huo uliofanyika Agosti 2024 mjini Harare, Zimbabwe, ambapo nchi wanachama zilitakiwa kuunga mkono wagombea wa kikanda kwa nafasi za juu katika AU.
SADC inaundwa na nchi 16, zikiwemo Angola, Botswana, Comoros, DRC, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Seychelles, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia, na Zimbabwe.
Endelea kufuatilia Nipashe Digital kwa taarifa zaidi kuhusu uchaguzi wa Mwenyekiti wa AUC.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED