Mwinyi: Bil. 300/- kutengwa kila mwezi kulipa deni la nchi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:44 AM Jan 04 2025
RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha: Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa serikali inatenga Sh. bilioni 300 kwa mwezi kulipa madeni ya nchi.

Aliyasema hayo jana alipofungua kituo cha mabasi kilichojengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF), eneo la Kijangwani, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema wakati serikali inakopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ina akaunti maalum inayoweka fedha za kutosha kwa ajili ya kulipa madeni hayo ambayo sasa inahifadhi ya Sh. bilioni 600.

Alisema deni hilo kwa upande wa Zanzibar kwa sasa ni Sh. trilioni 1.2 linalohimilika kwa kuwa serikali ina uwezo wa kulilipa ndani ya miaka miwili na kukopesheka tena kutokana na utaratibu uliopo.

Alisema wakati wa Serikali ya Awamu ya Nane deni hilo lilikuwa Sh. bilioni 800 ndani ya miaka minne limepanda na kufikia Sh. trilioni 1.2.

Aidha, aliwataka Wazanzibar kupuuzia taarifa zilizotolewa na vyama vya upinzani hivi karibuni kuwa deni hilo limefika Sh. trilioni 2.8 sawa na ongezeko la asilimia 208 akisema ni za upotoshaji na propaganda za kisiasa.

Alisisitiza kuwa serikali inakopa kwa nia njema ya kuendesha miradi ya maendeleo yenye tija na maslahi kwa nchi na sio vinginevyo.

Dk. Mwinyi pia alikemea urasimu unaofanywa na watu wasio waaminifu ndani ya serikali kwa taasisi binafsi zinazotaka kuwekeza nchini na kuzielekeza taasisi hizo kutoa taarifa kwake pale wanapokumbana na changamoto hiyo.

Akizungumzia kituo kipya cha mabasi, Dk. Mwinyi aliiagiza ZSSF kuwa na mpango maalum wa matunzo na usafi na kuandaa ajira maalum kwa vijana kwa ajili kutoa huduma za usafi.

Alisema serikali inatengeneza mpango mkuu wa usafiri utakaobadilisha mfumo wa sasa kuwa wa kisasa na kutoa huduma bora.

Alisema mpango huo utajumuisha ujenzi wa vituo vya kisasa vya mabasi katika maeneo ya Chuini, Jumbi Mwera, Mwanakwerekwe na Kijangwani, Malindi na Mnazi Mmoja kwa eneo la mjini.

Aidha, alisema kuwa kabla ya mwisho wa mwaka huu Zanzibar itaanza kutumia mabasi ya kutumia umeme.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Sada Mkuya Salum, alisema uwekezaji unaofanywa katika miradi mbalimbali nchini unaongeza thamani ya kiuchumi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Juma Malik Akili, alisema uchumi wa Zanzibar unategemea sekta za huduma hususan utalii na usafiri kwa asilimia 50.

Alisema pia mifumo ya kisasa ya usafiri inalenga kuviunganisha vijiji vyote vya Zanzibar na usafiri wa kisasa.

Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Nassor Shaaban, ameeleza kuwa zaidi ya Sh. bilioni 700 zimeingizwa sokoni na mfuko huo ili kuimarisha uchumi.

Alisema pia Sh. bilioni 250 zimelipwa kwa wastaafu ndani ya miaka minne ya awamu ya nane na wastaafu 15,000 wanaendelea kulipwa pensheni kwa mafanikio kila mwezi.