ASKOFU wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Mara, Dk. George Okoth, amewataka wazazi kuacha tabia ya kuwatelekezea walimu mzigo wa malezi ya watoto wao bali kuwekeza kwao malezi bora ili kuandaa taifa lenye maadili.
Askofu Okoth alitoa kauli hiyo juzi, akiwahubiria waamini wa kanisa hilo katika ibada maalumu ya kumbukumbu ya tohara na kubatizwa kwa Yesu Kristo.
“Wazazi wa kisasa wametingwa sana na shughuli za maendeleo yao wanafanya kazi, kwa hiyo basi jukumu la malezi ya watoto wamewasukumia walimu peke yao wanasahau kuwa ili mtoto aweze kukua ni lazima mwalimu afanye kazi yake na mzazi afanye jukumu lake la malezi ili mtoto awe raia mwema," alisema.
Aidha, alisema watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, mambo muhimu ya kuwarithisha ni pamoja na elimu dunia na kumjua Mungu.
Aliwataka wazazi kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha wanalea watoto wao kwa kuwa ni haki yao kupata malezi bora ili kuwaokoa katika matendo maovu yasiyoipendeza jamii na Mungu kwa ujumla.
Askofu Okoth, aliwakumbusha waamini wa kanisa hilo kukumbuka kumuomba Mungu awaongoze vyema katika kuita watoto majina yenye uhalisia wa malengo wanayotaka yatokee kwenye maisha yao.
Naye Mchungaji Baraka Ogina alisema, kanisa hilo limekuwa na desturi ya kuwahudumia watoto ambao wanaishi katika mazingira magumu kwa kuwakusanya pamoja kila Jumamosi na kuwapa mahitaji ya msingi ya chakula na mavazi.
“Tuna kituo cha huduma ya mtoto maarufu (Compassion) tuna watoto zaidi ya 250 ambao tuliwakusanya kwenye mitaa ya Manispaa ya Musoma kila Jumamosi wanakuja mafundisho na wanapata chakula cha asubuhi, mchana na jioni wanarudi kwenye familia zao."
Aliiambia Nipashe kuwa mafundisho wanayotoa kwa watoto hao ni neno la Mungu na elimu ya jamii na baadhi ya watoto wamesaidiwa kusoma elimu ya msingi, sekondari vyuo vikuu, vyuo vya kati na wengine wamepelekwa katika vyuo mbalimbali vya ufundi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED