Wakili Mwanaisha Mdeme atangaza kugombea Ubunge Kigamboni

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 07:53 PM Feb 07 2025

Katibu wa Idara ya Mambo ya Nje na Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara wa chama cha ACT-Wazalendo, Wakili Mwanaisha Mdeme.
Picha: Iman Nathaniel
Katibu wa Idara ya Mambo ya Nje na Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara wa chama cha ACT-Wazalendo, Wakili Mwanaisha Mdeme.

Katibu wa Idara ya Mambo ya Nje na Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara wa chama cha ACT-Wazalendo, Wakili Mwanaisha Mdeme, ametangaza azma yake ya kugombea ubunge wa Jimbo la Kigamboni katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Februari 6, 2025, Mdeme amesema ameamua kuingia katika kinyang'anyiro hicho ili kuwa sauti ya wananchi wa Kigamboni dhidi ya Serikali na kushughulikia changamoto zinazolikabili jimbo hilo.  

Amesisitiza kuwa, yeye pamoja na chama chake cha ACT-Wazalendo, watahakikisha wanatunga sheria zitakazowawezesha wananchi wote kufaidi rasilimali za taifa kwa usawa.  

Aidha, ameainisha vipaumbele vyake ikiwa ni kuboresha sekta ya afya, elimu, miundombinu, pamoja na kuinua vijana kiuchumi. Pia, ameahidi kutumia taaluma yake ya uwakili kushughulikia migogoro ya ardhi inayowakabili wakazi wa Kigamboni.  

Kuhusu Daraja la Mwalimu Nyerere, Mdeme amesema ni dhahiri kwamba daraja hilo ni kiungo muhimu kwa wananchi wa Kigamboni, hivyo si sahihi kwao kulazimika kulipia ili kulitumia. Ameahidi kuwa, endapo atachaguliwa, atafanya mazungumzo na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kubaini masharti ya mikataba iliyofikiwa kati yao na Serikali kuhusu daraja hilo.  

Vilevile, ameeleza masikitiko yake kuhusu uwepo wa kivuko kimoja tu cha Serikali, MV Kazi, huku kampuni ya Azam ikiendesha vivuko vinne. Ameeleza kuwa hali hiyo inawaathiri wananchi, hususan wanafunzi wanaolazimika kulipa shilingi 500 kuvuka bahari. Ameongeza kuwa, ubovu wa miundombinu katika baadhi ya maeneo ya jimbo hilo ni changamoto inayohitaji kushughulikiwa haraka.