MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Choma, Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama mkoani Shinyanga, amefariki dunia kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba aliyokuwa amepanga kutokana na mvua iliyonyesha saa saba usiku huku wenzake watatu wakijeruhiwa.
Mkuu wa Shule hiyo, Lucy Kibela alitoa taarifa hiyo jana wakati akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu juu ya tukio hilo, akisema nyumba nyingi ambazo wanafunzi wamepanga mitaani na vijijini si imara na zimejengwa kwa matofali ya udongo. Zinapoloa zinaanguka.
Alisema tukio hilo lilitokea saa saba Februari 5 mwaka huu, wanafunzi wanne walikuwa wamepanga katika chumba kimoja kwenye moja ya nyumba iliyoko jirani na shule hiyo.
Lucy alitaja mwanafunzi aliyefariki dunia kuwa ni Pendo Williamu (16) aliyekuwa akisoma kidato cha tatu na kwa majeruhi ni Sharida Shija (15) wa kidato cha kwanza, Neema Shija (16) wa kidato cha tatu na Regina Eliasi (16) wa kidato cha tatu.
"Wanafunzi watatu waliojeruhiwa na hali zao zinaendelea vyema na wameruhusiwa kurejea shuleni na niko nao, hali zao zikibadilika nitahakikisha wanawarejeshwa hospitalini. Suluhisho la janga hili ni kukamilisha ujenzi wa bweni la wanafunzi," alisema Mwalimu Lucy.
Alisema wazazi wengi wamewapangisha watoto wao mitaani jirani na shule kwa kuwa wengi wanatoka vijiji vya mbali ambako njiani wamekuwa wanakutana na changamoto mbalimbali, ukiwamo ubakaji na hivyo ili kuondoa adha hiyo, kuna haja kukamilisha ujenzi wa bweni shuleni.
“Kwa sasa kuna ujenzi wa bweni la wanafunzi lenye uwezo wa kubeba wanafunzi wa kike 80 na limejengwa kwa nguvu za wananchi na sasa lipo hatua ya lenta, tunaiomba serikali kuangalia namna ya kulikamilisha ili litumike na kuonda adha ya wanafunzi kuangukiwa na nyumba walizopanga mitaani," alisema Mwalimu Lucy.
Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kahama, ASP Stanley Luhwago alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa alipata taarifa na kufika eneo tukio na kubaini chanzo chake ni ukuta wa nyumba kutokuwa imara na kuangukia ndani ya chumba.
Alisema udhaifu wa ukuta huo ulisababishwa na mvua iliyokuwa inaendelea kunyesha wakati wa usiku, hivyo kusababisha kifo cha mwanafunzi huyo aliyefariki dunia papohapo.
ASP Luhwago aliwataka wakazi wa kata hiyo kujenga nyumba imara za matofali ya kuchoma badala ya udongo ambayo yakilowa yanapukutika, ili kuepukana na majanga ya namna hiyo.
Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita aliagiza Halmashauri kufanya ukaguzi wa nyumba hizo za watu binafsi wanaopangisha wanafunzi na kuhakikisha wanawahamisha waliomo katika nyumba mbovu na zisizo imara.
“Watoto wahamishwe na kupelekwa kwenye nyumba imara na salama kuepukana na majanga ya namna hii kwani nyumba nyingi vijijini zimejengwa kwa udongo, lakini nje zimepigwa plasta na kuonekana ni imara kwa nje, mvua inaponyesha saa 24 zinaanguka," alisema Mhita.
Mkuu wa Wilaya pia aliwataka madiwani kwenye maeneo yao kuwahamasisha wananchi kujenga nyumba za kisasa na kuachana na za udongo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED