HALI INATISHA GOMA; Wanawake wabakwa, wachomwa moto

By Moshi Lusonzo , Nipashe
Published at 10:17 AM Feb 07 2025
Wakazi wengi wamepoteza makazi
Picha: Mtandao
Wakazi wengi wamepoteza makazi

HALI ya kutisha imeukumba mji wa Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), baada ya maiti za watu kutapakaa katika mitaa mbalimbali baada ya kuuawa na waasi wa M23.

Katika tukio moja, waasi hao walivamia jengo la magereza na kisha kuwabaka wafungwa wanawake 160, wengi wao wamekutwa baada ya waasi kuchoma moto gereza hilo.

Vyumba vya kuhifadhi maiti vimefurika miili ya watu na mingine imerundikana nje kutokana na kuwepo kwa uhaba wa ardhi ya kuwazika.

Inaelezwa karibu watu 3,000 wameripotiwa kuuawa katika makabiliano ya silaha kati ya waasi wa kundi la M23 na wanajeshi wa DRC mashariki mwa nchi hiyo.

Mashirika ya kutoa misaada yalieleza miili ya watu waliouawa inatakiwa kuzikwa haraka iwezekanavyo kutokana na vyumba vya kuhifadhi maiti kufurika.

Katika taarifa yao, walisema hali inahatarisha na kuogofya.

Katika taarifa ya ndani ya Umoja wa Mataifa ambayo BBC ilipata nakala yake, inaonesha kuwa takriban wanawake 165 walishambuliwa wakati wa tukio la kutoroka kwa wafungwa wa kiume.

Idadi kubwa ya wanawake hao walifariki baadaye baada ya jela yao kuchomwa moto, ripoti hiyo ilieleza.

Hata hivyo, hali ya machafuko bado inaendelea katika mji wa Goma na hakuna dalili ya kurudi katika utulivu katika kipindi kifupi kijacho.

Kivu Kusini yashambuliwa

Waasi hao ambao wanaungwa mkono na Rwanda juzi waliuteka mji wenye madini wa Nyabibwe katika jimbo la Kivu Kusini.

Shirika la habari la Reuters liliripoti mapigano hayo yanajiri siku tano baada ya waasi hao kutanganza kusitisha mapigano.

Kutekwa kwa mji wa Nyabibwe unaopakana na Ziwa Kivu kunasababisha waasi kuwa karibu na mji mkuu wa jimbo hilo Bukavu.

Hata hivyo, wiki iliyopita waasi hao walisema kwamba hawana nia ya kuuteka mji huo.

Viongozi wa eneo hilo, wawakilishi wa mashirika ya kiraia, waasi na chanzo kutoka usalama wa taifa, wamethibitisha kuwa Nyabibwe iko mikononi mwa waasi wa M23.

"Kumekuwa na mapigano makali na mji uliangukia mikononi mwa waasi. Wako katikati mwa mji kwa sasa," alisema kiongozi huyo wa mashirika ya kiraia, ambaye kama vyanzo vingine hakutaka kutajwa jina lake.

Nyabibwe, kuna migodi ambayo huzalisha dhahabu, coltan na metali. Pia ni kitovu cha biashara kati ya Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini na Bukavu.

Waziri wa Mawasiliano wa DRC, Patrick Muyaya aliliambia shirika la habari la Reuters, kuwa waasi walikiuka usitishaji mapigano na wameingia katika mapambano na wanajeshi wa serikali karibu na Nyabibwe.

Corneille Nangaa, kiongozi wa muungano wa waasi wa Congo River Alliance unaojumuisha M23, alithibitisha kuwa kundi hilo limekwenda Nyabibwe.

 "Walitushambulia na sisi tukajilinda," aliambia Reuters.

Kwa upande mwingine, mahakama ya kijeshi ya Congo imetoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa Nangaa ikimtuhumu kwa uhalifu wa kivita na uhaini.

Malawi yaondoa jeshi, Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amemuagiza kamanda wa jeshi la nchi hiyo kujiandaa kuondoa majeshi ya Malawi kutoka eneo la Mashariki la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taarifa hiyo iliyotangazwa katika televisheni ya taifa, ilisema uamuzi wa rais unalenga kuheshimu tangazo la kusitisha mapigano kati ya pande zinazozozana.

Hata hivyo, uamuzi wa kusitisha mapigano uliotangazwa na Waasi wa M23 ulikuwa ni mpango wa kujipanga upya.

Kuondolewa kwa wanajeshi wa Malawi kutatoa nafasi ya mazungumzo yatakayo fanyika kesho ili kupata Amani ya kudumu.

Rais Lazarus Chakwera amekuwa chini ya shinikizo la kuondoa majeshi ya nchi yake Mashariki mwa DRC baada ya wanajeshi watatu wa Malawi kuuawa katika mashambulizi ya M23 mjini Goma.

Wanajeshi hao walikuwa sehemu ya ujumbe wa kulinda amani wa Kusini mwa Afrika uliotumwa na SADC kusaidia serikali ya Congo.

Makanisa yaomba amani

Wawakilishi wa Makanisa mawili makuu nchini, walisema hakutakuwa na suluhu ya mzozo huo ikiwa wahusika wakuu hawatajumuishwa katika kutafuta suluhu.

Wawakilishi wa Makanisa ya Kikatoliki na Kiprotestanti walitangaza kuanzishwa kwa mashauriano na wadau mbalimbali wa kisiasa, vyama vya upinzani, mashirika ya kiraia na waasi wa M23.

Mchungaji, Eric Nsenga, ambaye ni katibu mkuu wa Kanisa la Kristo nchini Congo (ECC), alisema jukumu la sasa linalotakiwa ni kukaa pamoja na kuzungumza.

“Jukumu letu sio kusema huyu ni malaika, yule ni shetani. Tunataka kupata suluhu, kwa hiyo sielewi kuwa tunazungumzia amani, lakini wakati huo huo tuna mashaka na utaratibu wowote unaoweza kuleta amani. " alisema mchungaji Nsenga.

Alisema katika mtazamo wao, wanalenga amani ya kudumu. Vyovyote iwavyo, itakuwa ni jambo la uwongo, kufikiria kuwa na amani bila kujumuisha wadau wote wanaohusika.

ICC yafuatilia karibu

Ofisi ya mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imesema inafuatilia kwa karibu hali inayoendelea nchini DRC, ikieleza kuwa vyanzo vya kuaminika vinaonesha kuwa mamia ya watu wameuawa katika ghasia zinazoendelea.

"Ofisi inafuatilia matukio ya sasa kwa karibu, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ghasia katika wiki za hivi karibuni mashariki mwa DRC, hasa ndani na karibu na Goma," ilisema katika taarifa yake.

Mwendesha Mashtaka wa ICC, Karim Khan, alitangaza kwamba Ofisi hiyo itarudia juhudi zake za uchunguzi nchini DRC, kwa kuzingatia madai ya uhalifu chini ya Mkataba wa Roma yaliyoripotiwa katika mkoa wa Kivu Kaskazini tangu Januari  1, 2022.

"Uchunguzi huu unaolengwa umeanzishwa na unaendelea kwa dharura," kilisema chanzo kimoja.

Vyanzo vya kuaminika vinaonesha kuwa maelfu ya watu wamejeruhiwa na mamia wameuawa ndani na karibu na Goma, wakiwemo raia na walinda amani katika mapigano hayo.