‘Bwala la Kidunda kumaliza uhaba wa maji Dar, Pwani’

By Christina Haule , Nipashe
Published at 05:15 PM Feb 07 2025
. Wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari, wakiwa katika picha ya pamoja walipotembelea Bwawa la Kidunda.
Picha: Christina Haule
. Wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari, wakiwa katika picha ya pamoja walipotembelea Bwawa la Kidunda.

MRADI wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda, linalojengwa mkoani Morogoro litakuwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita bilioni 190 za maji, umegharimu Sh. bilioni 336.

Kwa sasa, umefikia zaidi aslimia 27 za utekelezaji wake na mara baada ya kukamilika utaboresha huduma ya upatikanaji maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Akizungumza katika ziara ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), waliotembelea ujenzi wa mradi huo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Bwire Mkama, amesema bwawa la Kidunda litamaliza changamoto ya maji.

Mhariri Mtendaji wa gazeti la Nipashe, Beatrice Bandawe, akiwa anafuatilia maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Meneja Sehemu ya Mazingira na Uratibu wa Jumuiya za Watumia Maji kutoka Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Janeth Kisoma (hayumo pichani) kabla ya kutembelea Bwawa hilo.
“Jiji la Dar es Salaam, limekuwa likikutana na changamoto ya upatikanaji wa maji, hususani kipindi cha kiangazi, hivyo kukamilika kwa bwawa kutaboresha huduma ya majisafi na salama,” amesema.

Meneja Sehemu ya Mazingira na Uratibu wa Jumuiya za Watumia Maji kutoka Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Janeth Kisoma, amebainisha kuwa bwawa la Kidunda ni miongoni mwa vyanzo vya maji vinavyosimamiwa na Wami/Ruvu, huku akieleza mipango iliyopo ya kulitangaza kuwa eneo tengefu.

Aidha, Janeth amesema kuwa bodi imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali katika kuhifadhi mazingira na mpaka sasa zaidi ya Mabirika 29 ya kunyweshea mifugo yameshajengwa kwenye vijiji vinavyouzunguka Mto Ruvu, ili mifugo isiingie mtoni na kuharibu chanzo hicho.