MKUU wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita amewashauri wakazi wa Halmashauri ya Ushetu, kujenga nyumba imara na kuachana na za tope ambazo kwa kuwa ni hatari kipindi cha mvua.
Mhita aliyabainisha haya leo, wakati wa kikapo cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri hiyo cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Amesema nyumba nyingi vijijini zimejengwa kwa tope lakini nje zimepigwa plasta na kuonekana ni imara kwa nje, mvua inaponyesha saa 24 huanguka na kusabanisha vifo na kuwataka madiwani kwenye maeneo yao, kuwahamasisha wananchi kujenga nyumba za kisasa.
"Mwanafunzi wa kidato cha tatu sekondari ya Chona, amepoteza maisha kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba aliyokuwa amepanga na wenzake watatu jirani na shule, nyumba ingekuwa bora naimani isingeweza kuanguka," amesema Mhita.
Mhita amesema, kila mwananchi anaweza kujenga nyumba ya kisasa kwa kuwa wengi wao wanajihusisha katika kilimo cha mazao ya biashara na chakula, wakiuza na kupata fedha watenge kiasi, kwa ajili ya kujenga nyumba bora.
Hata hivyo amesema katika shule ambazo wanafunzi wamepanga kwenye nyumba za watu binafsi vijijini, halmashauri wakague nyumba walizopanga kama ni imara na kama watabaini ni mbovu wawahamishe na kuwapeleka sehemu salama.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Gagi Lala, amesema, watatumia mikutano yao ya hadhara katika kuwahamasisha wanachi kujenga makazi bora na kuachana na kujenga kwa tofarli za udongo, ambazo hazijachomwa.
Pia alisisitiza suala la wakuu wa idara kuzungukia shule zote za sekondari kufanya tathimini ya wanafunzi waliopanga kwenye mageto, kama nyumba hizo ni bora na imara.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED