Mbabe wa Yanga akaribia kutua KMC FC dirisha dogo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:48 AM Jan 04 2025
Mbabe wa Yanga akaribia  kutua KMC FC dirisha dogo.
Picha: Mtandao
Mbabe wa Yanga akaribia kutua KMC FC dirisha dogo.

KLABU ya KMC imetajwa iko katika mazungumzo ya kupata saini ya winga wa Azam FC, Cheickna Diakite, na Offen Chikola wa Tabora United kwa ajili ya kukiboresha kikosi chao kipindi hiki cha dirisha dogo.

Katika ushindi wa mabao 3-1 ambao Tabora United waliupata dhidi ya Yanga, Chikola alifunga magoli mawili.

Taarifa kutoka KMC FC zinasema klabu hiyo inawania saini za wachezaji hao ikiwa ni mapendekezo ya Kocha Mkuu, Kally Ongalla, ambaye anataka kukiongezea nguvu kikosi kwa kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa kutokana na ugumu wa ligi.

Chanzo kimesema KMC ina nafasi kubwa ya kumchukua Diakite, raia wa Mali, baada ya yeye mwenyewe kuomba atolewe hata kwa mkopo kwenda katika timu ambayo itampa nafasi zaidi ya kucheza kwa sababu kwa sasa amekuwa akisugua benchi kwenye kikosi cha Azam.

"Nadhani kwa Diakite ni rahisi zaidi kumpata kwa mkopo wa miezi sita, kwa sababu yeye mwenyewe amekuwa akishinikiza uongozi umtoe kwa mkopo kwa sababu amekuwa hapati nafasi ya kucheza, kwa upande wa Chikola, mazungumzo bado yanaendelea kwa sababu ni mmoja wa wachezaji tegemeo wa Tabora, hawawezi kumuachia kwa urahisi," kilisema chanzo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula, amesema kwa sasa hawezi kuwataja wachezaji wanaowahitaji  kipindi cha dirisha dogo la usajili ingawa taratibu za kusajili baadhi ya wachezaji kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi zimeshaanza.

"Tunataka kuboresha maeneo machache tu, hatutaacha wachezaji wengi,  watakaoingia ni vijana ambao tunaamini wana kiu na uchu wa kufikia mafanikio, tukikamilisha tutaweka wazi,” alisema Mwakasungula.

Mpaka Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama, ikiwa imemaliza mzunguko wa kwanza, KMC ipo nafasi ya 10, ikiwa imekusanya pointi 19, ikicheza michezo 16, ikipata ushindi mechi tano, sare nne na kupoteza michezo saba.