Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka mradi wa majiko ya gesi (LPG) ya kilo sita kwa bei ya ruzuku ya 50% kwa wananchi wa maeneo ya vijijini mkoani humo.
Ametoa shukrani hizo leo Januari 2, 2025 Ofisini kwake mkoani humo wakati wa utambulisho wa mradi na mtoa huduma atakayesambaza majiko hayo mkoani humo ambaye ni Kampuni ya Taifa Gas uliofanywa na Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emanuel Yesaya.
"Tumepokea mradi huu ambao unakwenda kusaidia kuondokana na athari za kiafya na pia utasaidia kuepuka vitendo vya kikatili, kulinda vyanzo vya maji na kutunza mazingira na pia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa inayosababisha mabadiliko ya tabia ya nchi," amesema Kanali Sawala.
Kanali Sawala ametoa wito kwa wananchi kuunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kununua majiko hayo ya ruzuku.
"Mhe. Rais anawapenda wananchi wake, ametuletea mradi nasi tuupokee na tumuunge mkono kwa kununua majiko haya ya ruzuku ili kulinda afya zetu sambamba na kuimarisha mazingira kama alivyoazimia," amesisitiza Kanali Sawala.
Aidha, ametoa wito kwa REA na Taifa Gas kuhakikisha wanashirikiana na viongozi katika maeneo yote ili waweze kuufahamu mradi na hivyo kurahisisha utekelezaji wake.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi, Mhandisi Yesaya amesema REA inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya Kupikia 2024-2024 kupitia programu mbalimbali ili kufanikisha azma ya Serikali ambayo muasisi wake ni Rais Dk. Samia Suluhu Hassan akiwa na lengo la kulinda afya za wananchi wake pamoja na kuhifadhi mazingira kwa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
"Tunaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ambao unaelekeza ifikapo mwaka 2034; asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi kupikia," amefafanua Mhandisi Yesaya.
Amesema jumla ya majiko ya gesi 16,275 ya kilo sita pamoja na vifaa vyake yatasambazwa katika wilaya tano za Mkoa wa Mtwara ambazo ni Mtwara, Masasi, Nanyumbu, Newala na Tandahimba ambapo kila wilaya itapata majiko 3,255 na mwananchi atalipia shilingi 19,500 tu na kwamba gharama nyingine imebebwa na Serikali.
Amesisitiza kuwa mtoa huduma atawajibika kusajili na kuandaa orodha ya wananchi watakaopatiwa majiko hayo. "Majiko haya yatauzwa kwa wananchi wenye vitambulisho vya NIDA au namba inayoweza kuhakikiwa; hakuna mwananchi atakayeruhusiwa kununua mtungi wa ruzuku zaidi ya mmoja," amesema
Kwa nyakati tofauti wananchi mkoani humo walimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea mradi huo na waliahidi kumuunga mkono kwa kuendelea kuhamasishana na kuelimishana ili kufikia azma.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED