LEO ni siku ya kupigakura kuchagua viongozi wa vitongoji, vijiji na mitaa baada ya wagombea kuhitimisha kampeni zao jana.
Ikumbukwe ni siku ya mapumziko na vituo vinafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 10 jioni, juu ya alama.
Tofauti na mwaka 2019, ambapo uchaguzi huo ulisusiwa, mwaka huu unashirikisha vyama 15 vyenye usajili wa kudumu ambavyo ni CCM, CHADEMA, ACT-Wazalendo, CUF, NCCR- Mageuzi, Demokrasia Makini, UMD, NLD na DP.
Ni kwa mujibu wa Msimamizi wa Uchaguzi TAMISEMI, Ummy Wayayu, akiongeza pia kuwa vipo SAU, UPDP, UDP, AAFP na ADC.
Jana wagombea na viongozi wa vyama hivyo walikuwa wakinadi sera za vyama vyao kwa wananchi kwenye maeneo mbalimbali tayari kwa kuchaguliwa leo.
Hata hivyo, baadhi ya vyama vinaingia kwenye kinyang'anyiro hicho vikiwa na malalamiko ya kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea wao katika vitongoji, vijiji na mitaa.
Pamoja na kuenguliwa, wapinzani wamekuja na mkakati ambao wanaamini utafanikisha kupata ushindi kwenye baadhi ya maeneo ambayo wagombea wao hawakuenguliwa au walienguliwa.
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam, jana anasema pamoja na baadhi ya wagombea wao kuenguliwa hawajakata tamaa.
"Tumetoa maelekezo kwa viongozi wetu ambayo tunaamini bado chama chetu kitashinda na pia upinzani utashinda iwapo uchaguzi utaendeshwa kwa uhuru na haki," anasema Dorothy.
Kiongozi wa chama anafafanua kuwa sehemu ambayo wagombea wao wameenguliwa, ACT-Wazalendo imeelekeza wanachama kupigia chama kingine cha upinzani chenye nguvu katika kitongoji, kijiji au mtaa.
"Hata kama atakuwapo mgombea mmoja wa upinzani asiye na nguvu, tutamuunga mkono tukiamini atashinda tu, lakini kikubwa zaidi ni kwamba kule ambako wapo CCM pekee yao, tutawapigia kura ya hapana kwani hatuungi mkono wanaotaka ushindi wa mezani," anasema.
Anaongeza kuwa huo ndio utaratibu wanaoingia nao kwenye uchaguzi wa serikali mwaka huu na kwamba kura za hapana zitaonyesha ni jinsi gani wananchi walivyochoka figisu za kuvuruga uchaguzi.
MKONO WA CUF
Naibu Katibu Mkuu CUF Bara, Magdalena Sakaya, anasema chama hicho kimetoa maelekezo kwa wanachama wake kupiga kura ya hapana kwa wagombea wa kijiji, kitongoji na mtaa ambalo wapinzani wameenguliwa."Tumetoa maelekezo hayo kwani maeneo mengi CCM imebaki pekee yake baada ya kuwaondoa wagombea wa upinzani. Nasi tumeona ni bora tufanye maamuzi hayo ili ikibidi uchaguzi urudiwe," anasema Magdalena.
Anaongeza kuwa kama wangekuwa wanakubalika wasingetumia mbinu za kuengua upinzani ili wabaki pekee yao, na kwamba kitendo hicho kinaonyesha ni jinsi gani wanavyohofia uchaguzi huo.
"Nchi hii ni yetu sote na si kwamba CCM ndio wenye uwezo wa kuongoza kuliko wengine. Kama wanakubalika kwa nini watumie mbinu hizo kwa lengo la kupata ushindi bila jasho?," Anahoji?
Magdalena anasema iwapo wanachama na wananchi wasio na vyama wakiamua kupiga kura za hapana kwa wagombea wanaotaka ushindi wa mezani, hatua hiyo itaonyesha ni jinsi gani wamechoshwa na mfumo uliopo.
Anasema wakati umefika kwa wananchi kuonyesha uamuzi wao kwa kuwachagua wale ambao wanawataka na kuwakataa wanaotaka kushinda kiulaini.
"Wananchi wasinyimwe uhuru wa kuchagua wagombea wanaowataka. Hivyo wito wangu kwao ni kwamba kila eneo ambalo wagombea wa upinzani wameenguliwa wapigiwe kura za hapana kwa sababu hakuna demokrasia," anasema.
Katibu mkuu huyo anasema katika vitongoji, vijiji na mitaa, wananchi wa maeneo hayo ndio wanaowajua wale ambao wanafaa kuwa viongozi wao, kutaka wasilazimishwe kuchagua watu fulani.
"Inawezekana wenzetu wameamua kuziba masikio ili wasisikilize ya wananchi wanawataka kina nani wawaongoze, lakini ukweli ni kwamba msingi wote wa uongozi si uongozi tu bali uongozi bora unaoweza kuleta maendeleo unaanzia kwenye serikali ya mtaa ambako wananchi wanachagua bila kuingiliwa kwani wanawafahamu wanaofaa," anasema.
HADI KIELEWEKE
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, anasema pamoja na changamoto za kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea wao, wameamua kukomaa hadi kieleweke na leo wanashiriki katika uchaguzi huo.Mnyika anasema wameamua kuendelea na uchaguzi huo tofauti na ule wa mwaka 2019 ulioipa CCM ushindi wa asilimia 90 licha ya kwamba baadhi ya wagombea wao wameenguliwa bila makosa.
“Kwa mfano, kati ya vitongoji 64,274, tumeachiwa wagombea 14,805, lakini pia kati ya vijiji 12,333 tumeachiwa wagombea 4,175, huku mitaa 4,269 tukiwa tumeachiwa mitaa 2,686 tu," anasema Mnyika.
Ni katika mkutano wake wa hivi karibuni na waandishi wa habari, mwenyekiti huyo anafafanua kuwa hata idadi hiyo ya wagombea wameipata baada ya kukomaa, vinginevyo wangeambulia wachache.
"Lakini pamoja na hayo, chama chetu hakijawahi kukubaliana kwa lolote kuhusu TAMISEMI kusimamia mchakato wa uchaguzi huo kuanzia uandikishaji ikiwamo ratiba ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania uongozi wa mtaa," anasema.
Anaongeza kuwa CHADEMA ‘inakomaa’ licha ya mchakato kuwa na changamoto kuanzia uandikishaji, kuchukua na kurejesha fomu hadi kuenguliwa au kuzuiliwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED