Waliofariki dunia Kariakoo wafikia 29

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 08:30 AM Nov 27 2024
Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba
Picha: Mtandao
Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba

WAKATI serikali ikitangaza kusitisha ubomoaji na kutafuta watu katika ghorofa lililoporomoka Kariakoo, Dar es Salaam,Novemba 16, mwaka huu, idadi ya watu waliofariki dunia wamefikia 29.

Miili mitatu ya waliofariki dunia kati ya tisa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzuru eneo hilo, haijatambuliwa na watu wawili waliojeruhiwa katika ajali hiyo bado wanaendelea na matibabu.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba, alisema jana kuwa hatua ya kubaini miili hiyo kwa njia ya vinasaba inaendelea. 

Akiwa katika eneo hilo, Makoba alisema kazi ya uokozi na kuitafuta miili zaidi ya watu waliopoteza maisha imesimamishwa rasmi, hivyo kuruhusu wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao kuanzia jana saa 8:00 mchana katika maeneo yote isipokuwa Mtaa wa Mchikichi. 

Makoba ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), alisema baada ya kumaliza hatua ya uokoaji kinachoendelea ni kuondoa kifusi chote na kukihifadhi sehemu maalumu huku uchunguzi wa kubaini chanzo cha ajali ukiendelea.

Pia alisema jambo lingine linalofuata ni serikali kwa kushirikiana na wafanyabiashara kwenda kuzitambua mali zao ambazo zimehifadhiwa na zinalindwa na vyombo vya dola.  

“Kamati ya maafa ya kitaifa ilipotokea maafa ilikuja kuweka kambi na sasa inakabidhi suala hilo kwa mamlaka za mkoa wa Dar es Salaam.  

“Kwa hiyo upande wa mtaa wa Manyema na Mchikichi unaoishia Congo na Mchikichi (eneo ambalo ghorofa limeporomoka) utafungwa kwa siku mbili tatu wakati shughuli za uchunguzi zinaendelea. Mitaa mingine yote serikali imeamua ifunguliwe wafanyabiashara waendelee na shughuli zao kama kawaida,” alisema Makoba.

Kuhusu wamiliki wa jengo hilo, alisema tayari wameshamtia nguvuni mmoja wa wamiliki na wengine wanaendelea kusakwa na Jeshi la Polisi huku uchunguzi ukiendelea.

“Kamati ya uchunguzi tayari imeshaanza kazi kwa hiyo tusiharibu uchunguzi,” alisisitiza Makoba.

SHANGWE WAFANYABIASHARA

Mfanyabiashara wa Nguo Kariakoo, Remsi Mbilu, alisema kitendo cha serikali kuruhusu maduka yaliyokuwa yamefungwa yafunguliwe katika eneo yalikotokea maafa ni jambo zuri.

“Mfano mimi nilikuwa ninategemea biashara ili maisha yangu yaende, sasa kwa hizi siku kumi nilikuwa ninaishi kwa tabu sana,” alisema.

Mfanyabiashara mwingine, Mahamudu Juma, alisema uamuzi wa kuwaruhusu waendelee na biashara una tija kwa kuwa maafa yameshatokea na kwamba huo ni mpango wa Mungu, hivyo  lazima shughuli nyingine ziendelee.