Aliyeshuhudia 'unga' atoa ushahidi kesi mume na mke

By Kulwa Mzee , Nipashe
Published at 12:15 PM Nov 27 2024
Sheria
Picha: Mtandao
Sheria

KOPLO Jackson Shambo (34) amedai alishuhudia unga uliokutwa nyumbani kwa mshtakiwa Samweli Kagisha na mkewe Brigitte Uwela ukifanyiwa uchunguzi na kubainika ni dawa za kulevya aina ya heroine.

Alidai hayo jana Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi wakati akitoa ushahidi mbele ya Jaji Sedekia Kisanya.

Shahidi huyo alidai kuwa Januari 31 mwaka huu, akiwa ofisini, alipewa taarifa na kiongozi wake Inspekta Johari kwamba anatakiwa kushuhudia ufunguaji wa kielelezo.

Alidai alielekezwa baada ya kufungua na kukifunga, anatakiwa kupeleka kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya uchunguzi.

Alidai alikwenda katika chumba cha kutunza vielelezo alikomkuta Inspekta Johari akiwa na washtakiwa wawili Samweli na Brigette, akaelekezwa kutafuta shahidi huru, alifanya hivyo akampata Julius Muzimu.

Alidai kuwa hatua ya kufungua kielelezo ilianza saa nane mchana ambapo Inspekta Johari alifungua bahasha ya kaki, ndani ikiwa na mfuko wa nailoni ang'avu ambao ndani yake mlikuwa na mfuko mweupe wa nguo ndani kukiwa na unga na chenga chenga zilizosadikiwa kuwa dawa za kulevya.

"Baada ya ufunguaji kukamilika, kielelezo kilifungwa, nilichukua na kukipeleka Ofisi ya Mkemia Mkuu, kilipokewa na Mkemia Emmanuel, niliongozana naye hadi maabara.

"Mkemia alichukua unga akaupima uzito, akapata gramu 978.42, alichukua sampuli kufanya uchunguzi wa awali, nilishuhudia uchunguzi maabara, baada ya uchunguzi aliniambia unga ule ni heroin," alidai.

Koplo huyo alidai alichukua sampuli nyingine kwa ajili ya uchunguzi zaidi na alimjulisha kwamba akimaliza ataandaa ripoti.

Alidai kuwa Februari 7 mwaka huu, alipigiwa simu kufuata ripoti ya uchunguzi.

Washtakiwa katika kesi hiyo wanadaiwa walikutwa na dawa hizo nyumbani kwao Shumbageni, wilayani Mkuranga.

Inadaiwa Januari 30 mwaka huu, Jeshi la Polisi lilipata taarifa kutoka kwa msiri kwamba watuhumiwa wanafanya biashara ya dawa za kulevya.

Baada ya kupewa taarifa hizo, inadaiwa askari wa jeshi hilo walifika nyumbani kwa watuhumiwa, wakafanya upekuzi na kukuta dawa hizo chumbani kwao.