MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameongoza wakazi wa mkoa huo kupiga kura kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa.
Kunenge amekuwa kati ya wananchi waliopiga kura katika kituo cha mkoani A ambao walifika na kupanga foleni kabla ya muda wa kuanza kupiga kura saa mbili asubuhi.
Nipashe Digital ilifika kituo cha mkoani A na kukuta tayari wananchi watano wapo kituoni wakisubiri muda wa kuanza kuingia kituoni kupiga kura.
Akizungumza baada ya kupiga kura Kunenge amesema hali ya usalama katika vituo vyote vya kupigia kura imeimarishwa na kwamba vituo vipo vya kutosha karibu na makazi ya watu.
Amesema wananchi wenye uchungu na maendeleo lazima watajitokeza kwa wingi kupiga kura kuchagua viongozi watakaoshirikiana nao .
"Kuna maeneo mengine watu hawapati haki ya kupiga kura nchini kwetu na katika mkoa wetu hali ni salama na amani imetawala kila mmoja kupata nafasi ya kupiga kura kuchagua kiongozi anayemtaka," amesema
Frida Matata ni mmoja ya waliojitokeza kupiga kura katika kata ya Tumbi ambaye amesema utaratibu wa kupiga kura uko vizuri na wananchi wanapiga kura bila usumbufu.
Mkoa wa Pwani una Vijiji 417, Mitaa 73 na Vitongoji 2028 sambamba na vituo 2,713 vya kupigia kura.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED