CHADEMA wakaa vituoni kulinda kura

By Paul Mabeja ,, Peter Mkwavila , Nipashe
Published at 04:13 PM Nov 27 2024
CHADEMA wakaa vituoni kulinda kura

BAADHI ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kata ya Chamwino jijini Dodoma, wamesema pamoja na kumaliza kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi wa mitaa yao hawataondoka kwenye vituo bali wataendelea kubaki ili kulinda kura zao.

Mmoja wa wafuasi wa Chama hicho, Kombo Adam Kombo, akizungumza Novemba 27,2024 na waandishi wa habari kwenye kituo cha kupigia kura Mtaa wa Mailimbili amesema wamekubaliana kutoondoka eneo hilo hadi matokeo yatakapo tangazwa.

“Sisi letu tupo hapa hatuondoki kwenda kokote ili kulinda kura zetu kama sharia inayotutaka manake wenzetu wamekuwa wajanja kuna mbinu amabzo zinafanyika ili kutuibia kura zetu sasa hatutoki leo hapa hadi kieleweke,”amesema

Akizungumza kuhusu mwenendo wa uchaguzi, amesema katika kituo hicho zoezi linakwenda vizuri kwani hakuna changamoto kubwa ambayo imejitokeza zaidi ya baadhi ya watu kukosa majina yao kwenye daftari.

“Mtaa wetu unavituo viwili hichi hapa cha Mailimbili pamoja na kile cha kwa Habiba ambacho ndicho kimeonekana kuwa na shida kwani kuna watu amabo wanakuja kupiga kura pasipokuwa na majina na sisi tumebaini watu hao na kuwakatalia kuingia kupiga kura,”amesema.

Naye, Rose Ibambilo amesema wameamua kubaki katika kituo hicho ili kulinda kura zao hadi hapo matokeo yatakapo tangazwa ili kuepuka wizi wa kura ambao umekua ukitokea kwenye uchaguzi kama huo mwaka 2019.

“Sisi tupo hapa kwa aamni kabisa tunashangaa watu wanazusha kuwa kunavurugu hadi askari polisi wanatumwa kuja kututisha lakini sisi tupo hapa kuanagalia kila kinachoendelea ili kulinda kura zetu na hatuta ondoka hadi kieleweke,”amesema Ibambilo.

Wakati huohuo, baadhi ya wakazi wa Jiji la Dodoma waliokuwa wamejiandikisha katika Daftari la Wakazi wamelalamika kukosa kuyaona majina yao na kusababisha kushindwa kutumia haki yao ya msingi.

Malalamiko hayo yametolewa na wakazi hao baada ya kufika kwenye vituo vyao walivyojiandikisha na kukosa kuyaona majina hayo japo kuwa waliandikishwa kwenye daftari hilo la mpiga kura. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Nipashe wananchi hao kwenye vituo mbalimbali vilivyopo ndani ya Jiji la Dodoma walisema kuwa kukosekana kwa majina yao kumewanyika haki yao ya msingi ya kupiga kura ambayo ingewapa viongozi wanaofaa kuongozi.

 Magreth Mathayo, kutoka mtaa wa Chadulu ameiomba serikali katika uchaguzi mkuu 2025 kwenye uandikishaji wa majina yaandikwe kwa kufuata herufi ili kuondoa kero hizo. 

"Tunaiomba serikali kuliangalia hili ili kuondoa usumbufu wa kuangalia majina yetu basi katika uchaguzi ujao wa Rais,Wabunge na Madiwani majina yetu yawekwe kwa kuafuata herufi ili iweze kuondoa malalamiko ambayo wengine yamesababisha kuyakosa majina yetu,"amesisitiza. 

Hata hivyo, pamoja na changamoto hizo zilizojitokeza bado wananchi hao wameipongeza serikali kutokana na amani na utulivu uliokuwepo kwenye uchaguzi huo ambao watu wametumia demokransia na kuweza kupiga kura bila kuhatarisha utulivu ulioopo. 

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Wakulima (AAFP),  Marck Mhomela, amelalamikia kitendo cha baadhi ya mawakala wao kuzuiliwa kuingia kwenye vituo vya uchaguzi. 

Amesema katika Kaya ya Makole, jiji hapa mmoja wa mawakala wao alikataliwa kuingia kwenye kituo cha uchaguzi hali iliyowalazimu kutumia nguvu ya ziada kupata kibali cha kuingia. 

“Tangu asubuhi majira ya saa 2:00 asubuhi uchaguzi umeanza lakini wakala wetu amekataliwa kuingia kwenye kituo hadi majira ya saa 7:00 mchana ndipo anapewa ruhusa ya kuongia kwenye kituo na uchaguzi ulishaa na watu wamepiga kura bila kuwepo kwa wakala wetu,”amesema.