"Watakaochezea SGR kukiona"

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:29 PM Nov 28 2024
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara.
Picha: Nipashe Digital
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara ametoa onyo kali kwa atakayebainika kuchezea miundombinu pamoja na treni ya SGR.

Aidha,amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote ambaye atahujumu miundombinu hiyo.

Profesa Kahyarara ameyasema hayo Novemba 27,2024 mara baada ya kutembelea Stesheni ya Samia Jijini Dodoma,kukagua shughuli mbalimbali za SGR.

Amesema mradi huo ni mkubwa na umeonesha manufaa makubwa kiuchumi kwani tangu Julai mwaka huu jumla ya wasafiri 1,029,540 walioingiza zaidi ya Sh.bilioni 28.5 wamehudumiwa.

"Tangu tumeanza huduma ya usafiri wa SGR tumeingiza Sh. 28,507,088,80,ni mafanikio makubwa huku matumizi yetu ya umeme yakiwa chini ya asilimia 10.

"Miundombinu hii ni yetu sote,inalindwa kwa sheria kali za reli na ile ya uhujumu uchumi.Tutazitumia ipasavyo kulinda huu mradi wa Watanzania,"amesisitiza.