MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), imeanza mchakato wa kuiongezea ‘hadhi’ Hifadhi ya Wanyamapori Makuyuni iliyoko mkoani Arusha.
Lengo ni kuwavutia watalii wengi zaidi hasa wakati wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) la mwaka 2027.
Makuyuni Wildlife Park, ambayo imeanzishwa mwaka huu, itakuwa na bustani ya wanyamapori ya kipekee katika nchi za Afrika, utalii wa night game drive, utalii wa ndege wa kipekee walioko eneo hilo, utalii wa kupanda balloon, utalii wa kutembea kwa kupanda milima, bush dinner, walking safaris na utalii wa kitamaduni.
Jana, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Dk. Simon Mduma, alisema hifadhi hiyo mpya itaongeza mapato kwa muda mfupi katika mashindano ya AFCON, ambapo Arusha itapokea wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali.
“Tumeanza rasmi utekelezaji wa mikakati ya kuiendeleza na kuiandaa Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park, kwa ajili ya kupokea wageni wengi zaidi, kwa kuongeza mindombinu ya utalii hususani barabara, ujenzi wa mabwawa ya maji na kuondoa mimea vamizi ndani ya eneo hilo.
"Mimi na bodi yangu, tumezunguka na tumeona maendeleo ya ujenzi wa barabara, ni kazi ambayo inaridhisha; ni nzuri na ratiba ambayo ipo kwa makubaliano kwenye mikataba kazi ya ujenzi wa barabara inaendelea vizuri sana," alisema.
Hifadhi hiyo imeanzishwa, baada ya Oktoba mwaka 2023, serikali kuyatwaa mashamba matatu makubwa, maarufu kama mashamba ya ‘STAIN’ yaliyokuwa yakimilikiwa na mwekezaji raia wa kigeni katika Wilaya ya Monduli.
Mashamba hayo ni Amani lenye ekari 9,007, Lente ekari 3,344 na Loldebes ekari 2,812, ambayo kwa sasa yanatumika kama eneo maalum la kuendeleza shughuli za uhifadhi na utalii.
Inaelezwa kwamba, uamuzi wa serikali ulichagizwa na hali ya utulivu wa mashamba hayo yaliyopo kwenye ushoroba unaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Manyara, Ranchi, Ziwa Manyara na Msitu wa Hifadhi wa Essimingor, ambao hupenda kutumiwa na wanyama kama eneo la mazalia.
Alisema: "Hifadhi hii ni mpya, ilikabidhiwa takribani mwaka mmoja uliopita, ilikuwa na uhitaji wa kuongeza barabara ili wageni watakaokuwa wanatembelea eneo hili, wawe na wigo mpana wa kuiona mandhari nzuri; na vilevile kutoa nafasi kubwa ya kuona vivutio ambavyo vipo kwenye hifadhi hii," alisema Dk. Mduma.
Aidha, Dk. Mduma, alisema eneo la Makuyuni kabla ya kutwaliwa, lilikuwa likikumbwa na changamoto ya ukame wakati wa kiangazi, kiasi cha kusababisha wanyamapori kutoka nje ya hifadhi hiyo na kwenda kwenye makazi ya watu.
“Bodi ya TAWA, iliona umuhimu wa kujenga bwawa la kukusanyia maji kwa ajili ya wanyamapori, hivyo bodi hiyo imefanya ukaguzi wa eneo litakapochimbwa bwawa hilo na kuridhishwa nalo na hivyo ujenzi wake utaanza hivi karibuni kwa kuwa mikataba imekwisha sainiwa tayari kwa kuanza kazi hiyo,” alisisitiza.
Mjumbe wa bodi hiyo, Prof. Suzanne Augustino, aliipongeza menejimenti ya TAWA kwa jitihada kubwa wanayoifanya kuboresha mazingira ya Makuyuni Wildlife Park, ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi ushauri na maelekezo yanayotolewa na bodi inayoongozwa na Mwenyekiti Meja Jenerali (mstaafu), Hamis Semfuko.
Naye Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, ambaye pia ni Kaimu Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini ya TAWA, Privatus Kasisi, alisema kitendo cha serikali kuiamini na kuikabidhi eneo hilo muhimu kumeipa chachu na nguvu ya kuliendeleza na kulisimamia kwa ukamilifu ili kulifanya liwe bora kwa manufaa ya wakazi wa Mkoa wa Arusha na taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Kamanda wa eneo la Makuyuni Wildlife Park, Andrew Kishe, aliieleza bodi hiyo kuwa miradi yote inayotekelezwa na TAWA ndani ya hifadhi hiyo inagharimu zaidi Sh. bilioni moja.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED