Makocha, waamuzi kunolewa Ruangwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:53 AM Nov 28 2024
Makocha, waamuzi kunolewa Ruangwa
Picha: Mtandao
Makocha, waamuzi kunolewa Ruangwa

WAZIRI Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Kassim Majaliwa, amesema atapeleka wakufunzi wa kuwanoa makocha wa timu za mpira wa miguu zilizoko katika jimbo hilo.

Majaliwa alisema hayo wakati akishuhudia mechi ya fainali ya Kombe la Jimbo (Jimbo Cup), iliyochezwa kwenye Uwanja wa Majaliwa ambapo Stand FC ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Kiongozi huyo alisema mashindano hayo yanatumika kuboresha maendeleo ya mpira wa miguu katika wilaya hiyo.

“Nitazungumza na Chama cha Makocha Taifa ili watupatie wakufunzi ambao watakuja kutoa mafunzo makocha wa Wilaya ya Ruangwa ya namna bora ya kusimamia timu zetu," alisema Majaliwa.

Aliongeza Ruangwa imeamua kujizatiti katika mpira wa miguu na kusema ni muhimu kuwa na waamuzi wenye uwezo mkubwa wa kusimamia michezo.

“Chama cha Mpira cha Wilaya orodhesheni marefa waliopo katika wilaya hii, nitaomba uongozi wa marefa tupate kiongozi mmoja ili aje aendeshe semina kwa marefa wetu,” aliongeza.

Katika hatua nyingine Majaliwa alisema  mashindano hayo yatasaidia kuongeza nguvu katika kikosi cha Namungo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Chama cha Mpira kimechagua wachezaji 18 kupitia michezo hii, nataka nimwagize mwenyekiti, wachezaji hawa waingie kambini mapema,” Majaliwa aliongeza.

Stand FC ilitwaa ubingwa baada ya kupata penalti 4-1 na kupata zawadi ya Sh. milioni tano, jezi seti mbili, mipira miwili pamoja na kombe huku mshindi wa pili akiondoka na Sh. milioni nne, mpira mmoja na jezi seti mbili.