MALALAMIKO ya kasoro katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa yametolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha ACT-Wazalendo, huku baadhi ya wapigakura wakiamua kulinda kura.
Vyama hivyo vimetafsiri kasoro hizo kuwa ni hujuma kwa kuwa wagombea pamoja na mawakala wao wanadaiwa kukamatwa vituoni na katika maeneo mengine kuchelewa kuanza upigaji kura kwa madai ya kuchelewa karatasi za kura au kuchanganya vitabu vyenye orodha ya wapigakura, vingine kupelekwa kituo A au B.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, alidai jana kuwa katika maeneo ya Chato, mjini Bariadi, mjini Kibaha, Msalala na Igunga, karatasi zilizokwisha kupigwa kura zilikamatwa.
"Katika eneo la Chato, karatasi za kura zilikamatwa kata ya Nyaruntembo, kijiji cha Nyantimba, kituo cha kupigia kura Nyantimba maboksi yenye kura ambazo zimeshapigwa tayari yamekamatwa kituoni na wananchi. Polisi wamefika na kuwakamata viongozi wetu na wameondoka na maboksi hayo yenye kura.
"Bariadi, kata ya Malambo, mtaa wa Nyashanda, zimekamatwa kura ambazo tayari zilishapigwa," alidai Mrema na kuongeza kuwa katika maeneo ya Msalala, kata ya Bugarama, kijiji cha Igudija, mpaka saa nne asubuhi jana upigaji kura ulikuwa haujaanza.
"Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Pwani, Bumija Senkondo amekamatwa, yuko ndani. Katika Jimbo la Segerea, kata ya Kisukuru, mtaa wa Kuhanga, karatasi za kupigia kura zimepelekwa mtaa wa Chanika, jimbo la Ukonga, Daftari la Wakazi lililopo kituoni hapo ni la mtaa wa Mainzini badala ya Luhanga, polisi wameitwa na wapo kwenye kituo hicho," alidai.
Alisema chama hicho kimeitaka Ofisi ya Rais - TAMISEMI itoe maelezo kwa umma kuhusu kura ambazo zilikamatwa tayari zimeshapigwa kwa wagombea maeneo mbalimbali ya nchi na hatua ambazo imepanga kuchukua dhidi ya wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo hayo.
Makamu Mwenyekiti wa ACT - Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, alisema uchaguzi umekumbwa na changamoto kubwa zinazotilia shaka uhalali wa mchakato huo.
Akizungumza baada ya kupiga kura katika mtaa wa Likotwa, mkoani Lindi, Mchinjita alitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukamataji kura feki, kuondolewa mawakala wa chama hicho kwenye vituo vya kupigia kura na kutokuwapo majina ya baadhi ya wagombea kwenye karatasi za kura.
Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema uchaguzi huo ni fursa kwa wananchi kupata viongozi wa karibu wanaoshughulikia changamoto za moja kwa moja katika maeneo yao.
Zitto alisema ushiriki wa kila raia ni muhimu katika kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanikiwa kwa haki na uwazi.
MATUKIO
Katika baadhi ya maeneo nchini, kumeripotiwa matukio yasiyo ya kawaida, ikiwamo baadhi ya wakazi kutoona majina yao, wasimamizi wa uchaguzi kutowasili kwa wakati vituoni, madai ya kuwapo kura feki na makada wa CHADEMA kuuawa.
Katika jimbo la Mikumi, wilayani Kilosa, kata saba zilichelewa kupiga kura kwa saa 2:30, kwa kile kilichoelezwa ni kuchelewa karatasi za kupigakura za wajumbe mchanganyiko wa serikali za vijiji na za wajumbe wa serikali za vijiji kundi la wanawake.
Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Mikumi, Ally Rashid, alisema jana kuwa hadi saa 4:30 asubuhi, kata zilizokuwa hazijaanza upigaji kura ni Ruaha, Ruhembe, Mabwerebwere, Masanze, Zombo, Tindiga na Kidodi.
Alidai kata tatu za Kilangali, Ulaya na Mhenda zilisimama kuendelea na uchaguzi kwa kile kilichoelezwa ni kuisha kwa karatasi za kupigia kura.
Katika Manispaa ya Musoma, mkoani Mara, wakazi wa vituo tofauti waliripotiwa kushindwa kupigakura baada ya kukuta majina yao hayasomeki vizuri, hali iliyowakatisha tamaa wengine na kulazimika kuondoka vituoni.
Mjini Tunduma, wilayani Momba, mkoani Songwe, kada wa CHADEMA, Steven Chalamila, aliripotiwa kushambuliwa kwa mapanga na kuuawa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake, usiku wa kuamkia jana.
Jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Jiji, Kiomoni Kibamba, alidai kuwa baadhi ya vijana katika kata ya Lwahnima, walivamia kituo cha kupigia kura za mwenyekiti na kutoweka nazo. Jitihada zilifanywa na watu hao walikamatwa.
Katika mtaa wa Sinza B, kata ya Sinza, wilayani Ubungo, Dar es Salaam, wakazi wa eneo hilo walilalamikia kuchelewa kubandikwa kwa majina yao nje ya kituo cha kupiga kura cha Shule ya Sekondari Mashujaa na baada ya kulalamika, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi walianza kuyabandika.
Mkoani Dodoma, iliripotiwa kuwa baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi walichelewa kufika vituoni, vikiwamo vya Ofisi ya Kata ya Chamwino na cha Nduka.
Mkoani Kigoma, mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mgera B, kata ya Mwandiga (CCM), Safiania Barikure, alikamatwa jana alfajiri kwa madai ya kukutwa na kura ambazo zilikuwa na mhuri wa Tume ya Uchaguzi.
Katika kituo cha Mlimwa, Dodoma, kuliibua mvutano kati ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Aisha Madoga na wasimamizi wa uchaguzi baada ya kubainika kuna mwananchi ambaye si mpigakura wa eneo hilo, amepiga kura bila kuonesha kielezo wala kuangaliwa katika daftari.
Madoga alipobaini hali hiyo alitishia kuondoka na daftari la wapigakura, lakini askari aliyekuwapo kituoni aliingilia kati na kumzuia.
"Nimekuja hapa na rafiki yangu ambaye si mkazi wa eneo hilo na hajajiandikisha kupiga kura katika mtaa huu, lakini cha kushangaza ameruhusiwa kupiga kura, huu si utaratibu uliowekwa, wanapaswa wasimamizi katika vituo waangalie majina ya watu kama yapo ndipo waruhusiwe kupiga kura," alisema Madoga .
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo mkoani Dodoma, Yohana Mussa alilalamikia mawakala wao kuzuiliwa kwa muda kuingia katika kituo cha kupigia kura Mtaa wa Mbuyuni, kata ya Kizota. Badala ya kuingia saa mbili asubuhi walidai kuruhusiwa kuingia saa tano asubuhi.
Msimamizi wa Uchaguzi Jiji la Dodoma, Dk. Fredrick Sagamiko, aliahidi kutoa ufafanuzi baadaye kwa madai kuwa alikuwa anazunguka vituoni kuangalia kinachojiri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi alipoulizwa kama kuna watu wanashikiliwa kuhusiana na uchaguzi huo, alisema hali ya uchaguzi ni shwari na suala la kura bandia hakuwa na taarifa nalo, akiahidi kufuatilia.
Mkoani Arusha, Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alidai chama hicho hakijatendwa haki katika baadhi ya maeneo, kwa kuwa mawakala wao walinyimwa nafasi ya kusimamia kwa muda mwafaka, badala yake walicheleweshwa kuanza kusimamia upigaji kura.
"Rafu ni nyingi tulizofanyiwa na Msimamizi wa Uchaguzi, sasa hatuelewi wanataka nani ashinde, wakati tunasema uchaguzi ni demokrasia, kwanini hatutendwi haki vyama vingine kama CHADEMA?" alihoji.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Murtallah Mbillu, alikanusha taarifa iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii kwamba polisi walisindikiza masanduku ya kura zilizopigwa wilayani humo.
"Taarifa sahihi ni kwamba wakala wa CHADEMA ambaye alitakiwa kuwa katika kituo cha kupigia kura cha Ndoinyo, kijiji cha Nasiporion, kata ya Endulen, tarafa ya Ngorongoro, alitakiwa kuwa katika kituo hicho saa mbili asubuhi, wakati wa kufungua kituo, yeye alifika akiwa amechelewa bila taarifa yoyote.
"Kwa vile muda wa kufungua kituo ili wananchi waanze kupiga kura ulishafika, upigaji kura ulianza. Alipofika ndipo akaanza kupiga picha na kuzituma anakofahamu yeye na waliotumiwa wakatengeneza taarifa hiyo ya uongo, wakiwa na lengo wanalolijua wao," alidai.
Baadhi ya wafuasi wa CHADEMA Kata ya Chamwino, jijini Dodoma walisema kuwa pamoja na kumaliza kupiga kura, hawataondoka vituoni, bali wataendelea kubaki ili kulinda kura zao.
Mmoja wa wafuasi wa chama hicho, Kombo Adam, akiwa katika kituo cha mtaa wa Mailimbili, alisema wamekubaliana kutoondoka eneo hilo hadi matokeo yatakapotangazwa.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Wakulima (AAFP), Marck Mhomela, alilalamikia kitendo cha baadhi ya mawakala wao kuzuiwa kuingia katika vituo vya uchaguzi.
Alidai kuwa katika kata ya Makole, jijini Dodoma, mmoja wa mawakala wao alikataliwa kuingia kituoni, hali iliyowalazimu kutumia nguvu ya ziada kupata kibali cha kuingia.
Mkoani Pwani, Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani humo, Bumija Moses pamoja na wakala wa chama hicho katika mtaa wa Mkongoni walishindwa kupiga kura baada ya kushikiliwa na polisi kwa saa sita, wakidaiwa kumfanyia fujo msimamizi wa uchaguzi.
Akizungumza baada ya kuachiwa kwa dhamana, mwenyekiti huyo alisema wakiwa katika kituo cha Mkongoni, msimamizi wa kituo alionekana akiwa na masanduku matatu yakiwa na kura ambazo tayari zimepigwa.
Alisema wananchi waliokuwa kituoni, walishangazwa na jambo hilo, hivyo walimpigia simu ili afike kufuatilia suala hilo na wakati anafuatilia ndipo alipoambiwa anafanya fujo na kupelekwa polisi akiwa na wakala wa CCM na CHADEMA.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, alisema jeshi hilo linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kufanya fujo kwa madai ya kutokuwa na imani na msimamizi wa kituo cha Mkongoni Kibaha.
Alisema uchunguzi wa awali umebaini walilenga kuharibu uchaguzi na kuleta taharuki kwa jamii.
*Imeandikwa na Elizabeth Zaya na Sabato Kasika (DAR), Paul Mabeja na Peter Mkwavila (DODOMA), Idda Mushi (Morogoro) na Julieth Mkireri (KIBAHA).
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED