Simba yatakata Afrika

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:20 AM Nov 28 2024
   Simba yatakata Afrika
Picha: Mtandao
Simba yatakata Afrika

BAO pekee lililofungwa na kiungo mshambuliaji wa kimataifa raia wa Ivory Coast, Jean Ahoua, liliipa Simba ushindi wa kwanza katika mechi ya raundi ya kwanza ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravo do Maquis ya Angola iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana.

Ahoua alifunga bao hilo dakika ya 26 kwa penalti baada ya beki wa Bravos do Maquis, Reuben Aderito, kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari wakati akijaribu kuokoa shambulizi kuelekea langoni kwao.

Awali krosi iliyopigwa na Ladack Chasambi, ilikuwa inakwenda katika kichwa cha Kibu Denis dakika ya 25, lakini beki  huyo aliokoa na mkono ili usimfikie winga wa Simba ambaye alikuwa amesharuka kichwa cha kuchumpa na mwamuzi, Ibrahim Mutaz kutoka Libya akaamuru pigo la  penalti.

Ahoua aliukwamisha wavuni na bao hilo likasimama hadi mwamuzi huyo alipopuliza filimbi ya mwisho kuashiria dakika 90 za mchezo huo zimemalizika kwa wenyeji kuondoka na pointi tatu muhimu.

Hata hivyo haukuwa ushindi rahisi kwa sababu dakika moja baada ya mapumziko, Bravo do Maquis, pia walipata penalti, baada ya Kibu kumkwatua, Emmanuel Edmond, akiwa katika harakati za kutaka kuuokoa.

Shujaa alikuwa ni kipa wa Msimbazi, Moussa Camara, alipofanikiwa kupangua penalti ya Edmond ambaye yeye mwenyewe alichukua jukumu la kupiga.

Camara alifanikiwa kuliweka salama lango la Simba alipookoa michomo mingi ya hatari kutoka kwa mastraika  wa Bravos do Maquis.

Hatari kubwa zaidi ilikuwa ni dakika ya 58, wakati Edmond alipobaki na kipa huyo akapiga shuti ambalo alilipangua, mpira ukaenda kwa Keoikantese Abednego, lakini alijitoa mzima mzima na kuokoa kwa mara ya pili mfululizo hali iliyosababisha aumie na kuomba msaada wa matibabu.

Katika mchezo huo, kila timu ilitawala kipindi kimoja, Simba ikitakata kipindi cha kwanza huku Bravos do Maquis wakifunguka kipindi cha pili kwa pasi za kuonana na kupiga mpira mirefu iliyoleta hatari zaidi langoni mwa wenyeji.

Simba ilifanya shambulio la kwanza katika lango la Bravo do Maquis, dakika ya sita, ambapo gonga za Ahoua na Chasambi zilimkuta Kibu akiwa katika  nafasi nzuri, lakini akapiga nje.

Simba ilirejea tena langoni mwa wageni wao dakika mbili baadaye, lakini shuti la Mganda, Steve Mukwala, akiwa nje ya eneo la 18 lilitoka nje.

Kibu angeweza kuipatia Simba bao dakika ya 15, lakini shuti lake dhaifu liliishia mikononi kwa kipa, Landu Mavanga.

Simba iliendelea kukosa mabao, Mukwala kwa mara nyingine, akiwa amemzidi nguvu na mbio beki, Samuel Bengue, akiwa peke yake na Mavanga alipiga nje huku mashabiki wakiwa wameshanyanyuka kujiandaa kushangilia.

Kipindi cha kwanza, Bravo do Maquis mara nyingi walikaa nyuma na mpaka dakika 45 zinamalizika hawakufanya shambulio lolote la maana, kabla ya kubadilika kipindi cha pili.

Timu zote zilifanya mabadiliko, Simba ikiwatoa Augustine Okejepha, Kibu, Ahoua, Mukwala na Chasambi, wakiingia, Debora Fernandes, Joshua Mutale, Leonel Ateba, Edwin Balua na Mzamiru Yassin, lakini matokeo hayakubadilika, badala yake timu zote zilishambulia kwa zamu na kukosa mabao.

Mechi nyingine ya Kundi A kati ya CS Sfaxien ya Tunisia na CS Costantine ya Algeria, ilitarajiwa kuchezwa jana usiku jijini Tunis.