UPIGAJI kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika jana, ulikwenda vizuri katika maeneo mengi huku baadhi ya maeneo ukikumbwa na kasoro zilizotia doa mchakato huo.
Huku upigaji kura ukifanyika kwa namna hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza matokeo yatakayotangazwa ni yale ya kura zilizohesabiwa kwenye masanduku ya kura na si vinginevyo.
AGIZO LA SAMIA
Akizungumza jana baada ya kupiga kura katika Kituo cha Sokoine, Kijiji cha Chamwino, Ikulu mkoani Dodoma, Rais Samia aliagiza kuwa matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa yatolewe kwa mujibu wa kura zilizopigwa kwenye masanduku ya kura.
"Watanzania wakapige kura kwa maelewano na masanduku ya kura yanavyosema ndivyo matokeo yatoke. Nimeona watu ni wengi wamejitokeza na kura hizi ni mtindo wa demokrasia na utamaduni wetu wa kisiasa. Waende kuufanya kwa usalama na kwa amani. Wasivunje amani yetu," alisema.
WALIOUAWA
Viongozi wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wamefariki dunia akiwamo mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Kitongoji cha Stendi, Kata ya Mkwese wilayani Manyoni, George Mohamed (41).
Pia Katibu wa CHADEMA, Jimbo la Singida Mjini, Hamis Nkua, amechomwa kisu kwenye bega akiwa Kata ya Mandewa na watu wanaodhaniwa ni makada wa chama (jina limehifadhiwa) kisha akakimbizwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Singida.
Jana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida lilisema linamshikilia Askari wa Jeshi Magereza kwa tuhuna za kusababisha mauaji hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Amon Kakwale, katika taarifa yake jana kwa vyombo vya habari alisema tukio la mauaji hayo lilitokea Novemba 25, mwaka huu, saa 5:00 usiku katika Kitongoji cha Stendi Kata ya Mkwese wilayani Manyoni.
Alisema chanzo cha mauaji hayo ni kwamba katika eneo la tukio, wafuasi wa CCM walikuwa katika nyumba moja wakifanya kikao cha ndani na ghafla walivamiwa na wafuasi wa CHADEMA, hivyo kusababisha vurugu.
Kamanda Kakwale alisema kutokana na vurugu hizo, askari magereza ambao wako eneo la Magereza walipigiwa simu kuhusu vurugu hizo na ikabidi waende kuona hali ilivyo huku wakiwasiliana na polisi.
Alisema askari walipofika eneo la tukio, walianza kushambuliwa kwa mawe jambo lililowalazimu kupiga risasi hewani kuwahadharisha na kuwazuia watu waliokuwa wakiwashambulia kwa mawe.
Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Manyoni, Danny Butale, akizungumza na Nipashe jana kwa simu akiwa njiani kwenda Tarime mkoani Mara, alisema tukio hilo lilitokea saa 7:00 usiku. Alisema mwili wa Juma ulipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni baada ya kuuawa.
Alisema kabla ya tukio kutokea, magari mawili yalifika usiku nyumbani kwa mgombea huyo na kuvamia kisha kumpiga risasi kiunoni na kupoteza maisha papo hapo.
Mkoani Songwe, kiongozi wa CHADEMA Jimbo la Tunduma, Steven Chalamila, alivamiwa nyumbani na kukatwakatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kufariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Augustino Senga, alithibitisha kifo cha Stephano Mwambeje (23) mkazi wa Chawa A Wilaya ya Momba kuwa alivamiwa na watu wasiojulikana na kukatwakatwa na kitu chenye kali kichwani na mikononi, hivyo kusababisha kifo chake.
Senga alisema Mwambeje alivamiwa usiku wa kuamkia jana majira ya saa 4:30 akiwa nyumbani kwake amelala baada ya watuhumiwa kuvunja mlango.
Alisema hadi sasa Jeshi la Polisi limemkamata mwanamume, dereva wa bodaboda kwa mahojiano ili kufahamu chanzo cha tukio hilo na wengine waliohusika ni kina nani.
JARIBIO KUCHOMA NYUMBA
Mkoani Rukwa, vijana waliovalia sare za chama kimoja cha siasa, wanadaiwa kuvamia nyumbani kwa Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CHADEMA), Aida Khenani, wakitaka kuchoma nyumba yake.
Khenani alisema vijana hao walikuwa wamebeba dumu lenye mafuta ya petroli na walidhibitiwa na wanachama wa CHADEMA waliokuwapo nyumbani kwake.
Inadaiwa tukio hilo lilitokea saa 4:00 usiku na kwamba pamoja na kuwa kwenye sare hizo hizo, pia walikuwa wakitumia pikipiki inayodaiwa ni mali ya chama hicho (kimehifadhiwa) yenye usajili Namba MC 992 EHY.
"Unajua hapa nyumbani pamoja na kuwa na familia yangu kwa maana ya mume wangu, pia walikuwapo baadhi ya mawakala na wagombea wengine wa CHADEMA wanaogombea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Tulikuwa tukiendelea na mazungumzo yetu ghafla tukasikia watu wakizunguka nyumba ndipo tulipojipanga na kufanikiwa kuwakamata," alisema.
Kwa mujibu wa Khenani, baada ya kuwakamata vijana hao na kuwahoji, walidai kuwa walitumwa na kiongozi mmoja wa juu wa serikali ngazi ya wilaya kwa nia ya kuiteketeza nyumba hiyo pasipo kujali ndani atakuwapo kina nani kwa kuwa yeye ndiye mlengwa mkuu.
Khenani alisema baada ya mahojiano na vijana hao waliokuwa wakiomba wasiuawe, alitoa taarifa polisi ambao walifika eneo la tukio na kuwakamata na kwenda kuwahoji na bado wanashikiliwa na polisi wilayani Nkasi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Shadrack Masija, alikiri kupata taarifa ya tukio hilo na kusisitiza atatoa taarifa yake kwa vyombo vya habari.
MAJINA KUKOSEKANA
Katika baadhi ya maeneo kulijitokeza kasoro kadhaa ikiwamo majina ya wapigakura kutokuonekana, hivyo kushindwa kupiga kura.
Baadhi ya maeneo hayo ni Tabata Liwiti na Shule ya Sekondari Migombani ambako majina ya wananchi hao, licha ya kujiandikisha, hayakuonekana katika sehemu zilizobandikwa.
Katika Kata ya Liwiti, mwandishi alishuhudia wananchi watano, akiwamo Joachim Mhagama kutoka kituo cha Zahanati ya NBC waliofika kupiga kura, lakini wakarudi nyumbani kwa shingo upande baada ya kutoona majina yao.
"Nimefika hapa kutimiza haki yangu ya kupiga kura lakini ndio hivyo nalazimika kurudi nyumbani kwa sababu jina langu halipo kwenye orodha ya waliojiandikisha,” alisema.
Mmoja wa wapigakura katika kituo cha Misewe, Ally Salehe, alimweleza mwandishi kuwa ametafuta jina lake kwa dakika 15 bila mafanikio, hivyo hakuona haja ya kuendelea kusubiri.
Katika kituo cha Segerea, uchaguzi wa Mtaa wa Migombani, uligubikwa na kasoro kadhaa zikiwamo wananchi kutokuona majina yao, watu kuingia kupiga kura bila kuona majina na kutokuhakikiwa kama ni watu sahihi kwa maana ya kukaguliwa vitambulisho vyao.
MCHEZO MCHAFU
Madai ya kuwapo vitendo vinavyoashiria kuwapo kwa ukiukwaji wa upigaji kura pia vilijitokeza.
Katika kituo cha Zahanati ya NBC, Liwiti, viongozi wa CHADEMA walikilalamikia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya vitendo kinyume cha sheria za uchaguzi, ikiwamo kuingiza wapigakura katika ofisi zao na baadaye kwenda kwenye eneo la kupiga kura.
Katibu wa CHADEMA Kata ya Liwiti, Stanley Mmanyi, alisema si sahihi wapigakura kuingia katika ofisi za CCM kwanza kisha kupiga kura kwa kuwa inaleta taswira ya kuibiwa kura.
Alisema anahisi walioingia katika ofisi hiyo sio watu wa mtaa huo bali wanakwenda kupewa majina ya watu hewa walioandikishwa ili watumie kupiga kura.
Alisema pia walikamata baadhi ya wagombea wa CCM, akiwamo anayegombea ujumbe wa serikali ya mtaa, Mussa Mwinjuma, wakibandika mabango ya kampeni jana asubuhi jambo ambalo ni kinyume na sheria za uchaguzi.
"Hata katika Mtaa wa Mfaume, leo asubuhi (jana) mtoto wa mgombea wa nafasi ya uenyekiti amekutwa akifanya kampeni nyumba kwa nyumba kuhamasisha watu wakampigie kura baba yake," alisema.
Aidha, kulikuwa na malumbano kati ya mgombea wa Uenyekiti Serikali ya Mitaa (CHADEMA), James Joseph, na msimamizi katika kituo hicho baada ya kutumia simu kufanya mawasiliano kinyume na sheria za uchaguzi.
Katika Kituo cha Liwiti, vitabu vya kupigia kura vilivyotumika awali vilikuwa vya kituo kingine, jambo lililogunduliwa na mgombea ujumbe kundi mchanganyiko kupitia tiketi ya CHADEMA, Oscar Njau, na kuutarifu uongozi na wakabadilisha vitabu hivyo.
Kasoro kama hizo pia zilijitokeza katika Kata ya Sokoni One, Arusha, baada ya baadhi ya wananchi kushindwa kupiga kura kutokana na majina yao kutokuwapo kwenye daftari.
Wananchi hao waliiambia Nipashe kuwa walijitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari kwenye kituo cha Logdong Kata ya Sokoni One lakini cha kushangaza jana majina yao hayakuwapo na waliyoyakuta ni ya watu wengine kabisa.
Katika Kituo cha Engasengiu, Kata ya Sinoni, mgombea wa nafasi ya mwenyekiti, Damiano Mollel (CHADEMA), aliangua kilio baada ya kukosa jina lake kwenye kituo cha kura, kitu ambacho alidai ni hujuma zimefanyika dhidi yake.
MAWAKALA WAZUIWA
Baadhi ya maeneo jijini Arusha, kumekuwa na mvurugano na sitofahamu kutokana na mawakala wa vyama vya upinzani kutokuwapo katika vituo vya kupigia kura hasa Kata ya Unga Limited.
Akizungumzia hali hiyo, Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Arusha, John Kayombo, alisema vyama 12 vimechukua fomu na wasimamizi wao na kula kiapo isipokuwa CHADEMA pekee.
"CHADEMA waliweka mawakala wengi, yaani unakuta kituo kimoja mawakala watano au watatu kitu ambacho ni kinyume na utaratibu. Tuliwaita waje wapunguze baadhi ya mawakala na wabaki wale wanaohitajika lakini hadi jana (juzi) jioni walikuwa bado wana mvutano na hakuna hadi sasa waliokula kiapo," alisema Kayombo.
Aidha, katika Mtaa wa Nado Kati, Kata ya Muriet, masanduku ya kupigia kura yalichelewa kufika hadi saa 4:00 asubuhi. Katika Mtaa wa Muriet Mashariki, masanduku ya kura yalifika majira ya saa 09:30 asubuhi.
Kutokana na kasoro hizo, mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Makongoro, Albert Makingile (CCM), alishauri kuwa kuna haja serikali kutoa namba kwa kila raia, ambazo zitawezesha kutambua jina lake kwa haraka.
MWAMKO MDOGO
Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo, alisema mwamko mdogo wa vijana katika upigaji wa kura umechangiwa na baadhi yao kutotulia mahali pamoja kutokana na shughuli za utafutaji.
Mkoani Tanga, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainab Abdallah Issa, baada ya kupiga kura katika Ofisi ya Mtendaji Kata ya Mbaramo, aliwasihi wananchi wapige kura mapema na wasibubiri dakika za lala salama.
· Imeandikwa na Godfrey Mushi, Cynthia Mwilolezi (Arusha), Mary Mosha (Moshi), Oscar Assenga (Tanga),Mussa Mwangoka (Katavi), Jenipher Gilla (DAR) na Thobias Mwanakatwe (SINGIDA).
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED