JIJI la Mbeya limetajwa miongoni mwa maeneo ambayo wananchi wake wanatumia kiwango kikubwa cha mkaa kwa ajili ya kupikia, hali ambayo inachangia uharibifu wa mazingira hasa ukataji wa misitu katika maeneo mbalimbali.
Kamishna Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu nchini (CC), Prof. Dos Santos Silayo aliyasema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa upandaji miti kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya ikiwemo kwenye vyanzo vya maji na kwenye taasisi za elimu.
Alisema takwimu zilizopo ni kwamba wananchi wa Jiji hilo wanatumia kiwango kikubwa cha mkaa ambao unachomwa katika Wilaya za Chunya, Songwe na maeneo mengine ya jirani.
Aliwataka wananchi wa Jiji hilo kubadilika na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi ili kupunguza kiwango cha uharibifu wa mazingira kwenye maeneo hayo pamoja na kulinda afya za wananchi.
Alisema uharibifu huo wa mazingira unasababisha mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kupungua kwa kiwango cha mvua na kuongezeka kwa joto duniani.
Aliipongeza taasisi ya Tulia Trust ambayo inaongozwa na Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson kwa kujitolea miti hiyo ambayo itapandwa kwenye maeneo mbalimbali kwa lengo la kulinda mazingira.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Dk. Tulia alisema taasisi yake ilianza kutoa miti hiyo zaidi ya miaka miwili iliyopita ambapo ilianza na miti ya matunda ambayo ilikuwa inatolewa bure kwa wananchi kwa ajili ya kupanda kwenye makazi yao.
Alisema lengo la taasisi hiyo ni kupanda zaidi ya miti 2,000,000 na kwamba kwa mwaka huu wanatarajia kupanda miti 2,000 kwenye maeneo mbalimbali hasa kwenye vyanzo vya maji na kwenye shule mbalimbali za msingi na sekondari.
Alisema mbali na maeneo hayo pia watapanda miti hiyo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na maeneo yote ya wazi ili kuhakikisha yanakuwa salama.
Aliwataka wadau wengine wa mazingira kushiriki katika kupanda miti kwenye maeneo yote ya wazi ili kuhakikisha maeneo yote ya wazi yanakuwa safi.
Diwani wa Kata ya Mwakibete ambako upandaji huo wa miti ulizinduliwa, Lucas Mwampiki alisema watahakikisha wanailinda miti hiyo ili istawi na kutimiza azma ya serikali.
Pia, aliwataka wananchi wa kata hiyo kushiriki kwenye upandaji wa miti na kuitunza na kwamba kila mwananchi anatakiwa kushiriki kuipanda na kuitunza ili istawi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED